Pata taarifa kuu
TANZANIA-JOHN MAGUFULI

Vilima vya Kola, eneo linalohifadhi Kumbukumbu ya ajali ya mlipuko wa gari la mafuta Morogoro

Agosti 10 mwaka 2019 itasalia kumbukumbu mbaya kwa wakazi wa eneo la Msamvu Mkoani Morogoro, baada ya kutokea ajali ya mlipuko wa gari la mafuta, ajali iliyosababisha zaidi ya watu 100 kupoteza maisha.

Mwanahabari wa RFI Kiswahili Fredrick Nwaka (kulia) akiwa katika eneo la Kolla Mkoani Morogoro
Mwanahabari wa RFI Kiswahili Fredrick Nwaka (kulia) akiwa katika eneo la Kolla Mkoani Morogoro RFI/Fredrick Nwaka
Matangazo ya kibiashara

Majeruhi wa ajali hiyo walilazwa katika hospitali ya mkoa wa Morogoro na wengine kusafirishwa katika hospitali ya kitaifa ya Muhimbili iliyopo mji mkuu wa kibiashar wa Dar es Salaam kwa ajili ya matibabu zaidi.

Rais wa Tanzania John Magufuli alitangaza siku tatu za maombolezo sanjari na kuwatemebela majeruhi wa ajali hiyo na pia alitangaza serikali yake kugharamia matibabu ya watu wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo.

Mwanahabari wa RFI Kiswahili, Fredrick Nwaka alifika eneo la vilima vya Kolla Septemba 4, karibu zaidi ya wiki tatu tangu kutokea kwa tukio hilo ambalo lingali na simanzi kwa wakazi wa eneo la Msamvu na Morogoro kwa ujumla waliopoteza jamaa zao.

Ni eneo kubwa ambalo pia hutumiwa kwa mazishi lakini watu waliokufa kwa ajali wametengwa katika eneo moja.

Awali niliogopa kuwa eneo hilo kwa kuwa ni tukio ambalo binafsi liliusisimua sana mwili wangu, ni tukio la kusikitisha na lililondoa uhai wa watanzania wengi vijana kwa wakati mmoja.

Mbali na kujionea eneo walipozikwa watu waliopoteza maisha pia kungali na makaburi mengine ambayo bado hayajazikwa na nilipomuuliza mmoja wa watu eneo hilo akasema majeruhi yeyote wa ajali atakayepoteza maisha atazikwa eneo hilo.

Makaburi hayo yanatambuliwa kwa namba ili kurahisiwa utambuzi wa makaburi wa ndugu zao.

Mzee mmoja aliyeondokewa na mdogo wake aliniambia hadi sasa bado hajatambua kaburi la nduguye licha ya kukamilisha taratibu zote za utambuzi.

Hata hivyo anasema bado ana matumaini ya kutambua kaburi la nduguye kulingana na utaratibu uliowekwa na serikali ya mkoa.

Ni wazi eneo hilo linatasalia kumbukumbu muhimu kwa kizazi cha sasa na kijacho na kwangu binafsi. Mwenyezi Mungu azilaze mahala pema roho za marehemu na pia nafuu kwa majeruhi wote wa ajali ambao wangalia wanapatiwa matibabu.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.