Pata taarifa kuu
BURUNDI-KATIBA-SIASA-USALAMA

Wananchi wa Burundi wanapiga kura kuhusu mabadiliko ya Katiba Alhamisi

Wananchi wa Burundi wanapiga kura ya maoni Alhamisi hii Mei 17 kuibadilisha Katiba ya nchi hiyo. Iwapo Katiba itabadilishwa, huenda rais Pierre Nkurunziza akaendelea kuwa madarakani hadi mwaka 2034. Je, Burundi ilifikaje hapa ?

Kura ya Ndiyo ikipita kuhusu mabadiliko ya Katiba Pierre Nkurunziza (kwenye Picha) anatarajia kuongoza Burundi hadi mwaka 2034
Kura ya Ndiyo ikipita kuhusu mabadiliko ya Katiba Pierre Nkurunziza (kwenye Picha) anatarajia kuongoza Burundi hadi mwaka 2034 © RFI-KISWAHILI
Matangazo ya kibiashara

Serikali ya Burundi ilipata wazo la kuibadilisha Katiba ya nchi hiyo baada ya jaribio la mapinduzi ya kijeshi dhidi ya rais Piere Nkurunziza mwaka 2015 ambalo halikufanikiwa.

Haya yote yalikuja, baada ya rais Nkurunziza kutangaza kuwa angewania urais kwa muhula wa tatu licha ya pingamizi kutoka kwa wapinzani wake.

Upinzani ulisisitiza kuwa rais Nkurunziza alikuwa amehudumu kwa mihula miwili na muda wake wa kuondoka ulikuwa umefika kwa mujibu wa katiba na mkataba wa amani wa Arusha.

Hata hivyo, Nkurunziza alisema muhula wake wa kwanza ulianza mwaka 2010 wala sio mwaka 2005 kwa sababu, wakati huo alichaguliwa na wabunge wala sio wananchi.

Watu 1,200 walipoteza maisha katika mzozo wa kisiasa uliochukua miezi kadhaa, huku wengine wakikamatwa na wengine kutoweka.

Wanasiasa wa upinzani, wanahabari na wanaharakati waliikimbia nchi hiyo kwa hofu ya kukamatwa au kuuawa na maafisa wa usalama.

Mwezi Julai mwaka 2016, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha azimio la kuwatuma polisi 228 wa Kimataifa nchini humo lakini serikali ya Burundi ilikataa.

Katika kipindi hicho pia, Burundi ilitangaza kuwa inajiondoa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC baada ya kushtumiwa kuwa inakiuka haki za binadamu.

Kuelekea upigaji kura hapo kesho, mamia ya wapinzani wa rais Nkurunziza bado wanazuiwa na mapema mwezi huu, serikali ya Bujumbura ilitangaza kuzima mitambo ya vituo vya redio vya Kimataifa vya BBC na VOA kwa madai ya kupeperusha taarifa za uongo na zinazotishia usalama wa nchi hiyo huku Radio France International ikionywa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.