Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA-UCHAGUZI

Rais Kenyatta asema atakuwa rais wa wote, awaomba wapinzani kuungana naye

Rais Uhuru Kenyatta ameapishwa kuiongoza Kenya kwa muhula wa pili na wa mwisho baada ya Uchaguzi wa urais mwezi uliopita. Sherehe za kumwapisha rais Kenyatta na naibu wake William Ruto, zilifanyika katika Uwanja wa Kimataifa wa Michezo wa Kasarani jijini Nairobi na kuhudhuriwa na maelfu ya wananchi.

Rais Uhuru Kenyatta akila kiapo kuongoza Kenya kwa muhula wa pili katika uwanja wa Michezo wa Kasarani jijini Nairobi, Novemba  28, 2017.
Rais Uhuru Kenyatta akila kiapo kuongoza Kenya kwa muhula wa pili katika uwanja wa Michezo wa Kasarani jijini Nairobi, Novemba 28, 2017. REUTERS/Thomas Mukoya
Matangazo ya kibiashara

Wageni wengine mashuhuri kutoka mataifa 40, wakiwemo marais kutoka mataifa ya Afrika wakiongozwa na rais wa Uganda Yoweri Museveni, Paul Kagame wa Rwanda, Edgar Lungu wa Zambia, Ali Bongo wa Gabon miongoni mwa wengine, walihudhuria sherehe hizo.

Rais Kenyatta ameahidi kuilinda na kuihifadhi Katiba ya nchi ya Kenya, katika kipindi cha miaka mitano atakapokuwa madarakani.

"Mimi Uhuru Kenyatta, naapa kuwa nitakuwa mwaminifu kwa Jamhuri ya Kenya, nitaiheshimu, nitailinda, kuitetea na kuihifadhi Katiba, Mungu nisaidie," alisema Kenyatta.

Katika hotuba yake, rais Kenyatta amesema atakuwa rais wa Wakenya wote, waliompigia kura na wale ambao hawakumpigia.

“Nitakuwa rais wa wote, nitatumia muda wangu kujenga madaraja ili kumfikia kila mmoja,” alisema Kenyatta.

“Uchaguzi sasa umekwisha, tumemaliza mzunguko wote kufikia leo,” alisisitiza Kenyatta.

“Kila mmoja katika nafasi yake, afuate katiba na sheria kama inavyoeleza,” aliongeza.

Aidha, amesema kuwa katika uongozi, utachukua mawazo ya wapinzani wake ili kuyafanyia kazi kwa kile alichokisema kuwa nao walikuwa na nia ya kuiongoza nchi.

Rais wa Uganda ambaye pia ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Yoweri Museveni, ametoa wito kwa Wakenya kuacha kulinda amani na kuacha siasa mara kwa mara.

“Naomba Wakenya wote wakumbuke mambo matatu au manne muhimu, jambo la kwanza ni amani, jambo la pili ni ustawi wa Jamii, jambo la tatu ni maendeleo na jambo la nne ni siasa msifikirie sana siasa mkasahau haya mengine matatu,” alisema Museveni huku akishangiliwa.

Akizungumza kwa niaba ya wageni mashuhuri, rais wa Zambia Edgar Lungu, amewaaambia Wakenya kurudi kazini baada ya kumalizika kwa zoezi la Uchaguzi.

“Hongereni sana, kwa hatua hii, tulikuwa na wasiwasi kuwa hali hii ingechukua muda mrefu lakini sasa hili limeisha,” alisema.

Naye rais wa Rwanda Paul Kagame aliwapongeza Wakenya kwa kumaliza zoezi la Uchaguzi.

“Hongereni sana Wakenya,” alisema.

Kiongozi wa muungano wa upinzani nchini Kenya NASA Raila Odinga amesisitiza kuwa, hatambui utawala wa rais Kenyatta.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.