Pata taarifa kuu
KENYA-SIASA

Kenya: Bunge la Seneti laidhinisha muswada wa sheria tata ya Uchaguzi, rais Kenyatta asubiriwa kutia saini

Maseneta kutoka chama tawala nchini Kenya, Jubilee, Alhamisi ya wiki hii waliondoka kwenye ukumbi wa mikutano huku wakiwa wamefanikiwa kupitisha muswada wa sheria tata ya uchaguzi bila kufanyiwa marekebisho, hatua inayotoa nafasi kwa rais Uhuru Kenyatta sasa kutia saini muswada huo kuwa sheria. 

Wabunge wa Seneti nchini Kenya wakionekana wakati wa mjadala wa kupitisha sheria tata ya uchaguzi, 5 Januari, 2017.
Wabunge wa Seneti nchini Kenya wakionekana wakati wa mjadala wa kupitisha sheria tata ya uchaguzi, 5 Januari, 2017. YouTube/Shot/KTN
Matangazo ya kibiashara

Muswada huu wa mabadiliko ya sheria ya uchaguzi, umepitishwa licha ya juhudi zilizooongozwa na kiongozi wa wachache bungeni, seneta Moses Wetang'ula, aliyedai kuwa muswada uliopitishwa ni kinyume cha katiba na unaweza kuiingiza nchi hiyo kwenye machafuko.

Akizungumza wakati akichangia seneta Wetang'ula, aliwataka wabunge wenzake kutumia busara wakati watakapopiga kura na kuwataka waoneshe wananchi wa Kenya kuwa, baraza la seneti linafuata misingi ya demokrasia.

"Fanyeni kila mnachoweza lakini msitake kuichafua nchi yetu. Hebu tuwe makini na tujaribu kunusuru picha ya bunge hili," alisema seneta Wetang'ula.

Hata hivyo maseneta wa Jubilee, ambao walionekana wazi kutokuwa tayari kuchelewesha mchakato huo kwa kutaka kubadilishwa kwa baadhi ya vipengele, huku wakitumia idadi kubwa ya wabunge wao kupitisha muswada huo.

Licha ya majibizano na ushawishi mkubwa wa wabunge wa upinzani, wabunge 26 walipiga kura kuunga mkono muswada huo huku wabunge 10 wakiupinga, kura iliyotoa pigo kwa wabunge wa upinzani.

Tayari vinara wa muungano wa upinzani wa CORD wameanza kukutana na huenda wakatoa tamko lao hivi karibuni kuhusiana na kile kilichokubaliwa bungeni.

Tarehe 4 ya mwezi Januari mwaka huu, viongozi wa upinzani walitangaza kusitisha maandamano yao kupinga sheria hii kwa kile walichosema wanatoa nafasi ya kufanyika kwa mazungumzo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.