DRC: Mji wa Kalemie washuhudia mafuriko yanayotokana na mvua kubwa
Mvua kubwa inayoendelea kunyesha imesababisha mafuriko na kukwamisha shughuli za kawaida, kwenye mji wa Kalemie nchini DRC, huku kiwango cha maji katika Ziwa Tanganyika, kikiongeka.
Imechapishwa:
Cheza - 01:17
Watu zaidi ya Elfu tatu wameyakimbia makaazi yao huku miundombinu ikiharibika.
Mji wa Kalemie umegawanyika kwa sehemu mbili, Barabara ya Lumumba ambayo ni barabara kuu inayounganisha sehemu ya mji na mtaa wa Lukuga, inafunikwa na maji kwa zaidi ya mita 100.
Magari machache tu ndio bado yanajaribu kutumia barabara hii, wakati huu baadhi wakilazimika kuvuka kwa kutumia mtumbwi.
Mbali na kuongezeka kwa viwango vya maji katika Ziwa Tanganyika, mito inayozunguka mji wa Kalemie,nayo pia imefurika. Kwa mujibu wa mashirika ya kiraia, zaidi ya jamaa 3,500 wameathirika na janga hili.
Soma piaDRC: Takriban watu 8 wafariki kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha Kinshasa
Idadi ya wanaothirika na mafuriko haya inaendelea kuongezeka wakati hii familia nyingi zikiyahama makazi yao. Baadhi ya miundombinu kama vile hoteli na shule zimeharibiwa .
Jules Mulya, kiongozi wa wafanyibiashara katika eneo hili , anaeleza kuwa shughuli za kiuchumi pia zinaathirika. Nyumba nyingi za biashara zimefurika maji.
Kwa upande wake, waziri wa miundombinu wa jimbo hilo, John Seya, ameeleza kuwa jimbo la Tanganyika halina uwezo kifedha wa kukabiliana na janga hili.
Denise Maheho- Lubumbashi.