Pata taarifa kuu

Kenya itatekeleza jukumu lake la polisi nchini Haiti mara tu baraza la rais litakapowekwa

Rais wa Kenya William Ruto amesema Jumatano kwamba ameihakikishia Marekani kwamba kutumwa kwa maafisa wa polisi nchini Haiti kunakopangwa kama sehemu ya ujumbe wa kimataifa unaoongozwa na Nairobi kutafanyika wakati baraza la mpito la rais litakapoundwa kisiwani humo.

Wapita njia wakipita karibu na gari la polisi huko Port-au-Prince, Haiti, Alhamisi, Machi 7, 2024, wakati mashambulizi ya magenge yakizorotesha nchi.
Wapita njia wakipita karibu na gari la polisi huko Port-au-Prince, Haiti, Alhamisi, Machi 7, 2024, wakati mashambulizi ya magenge yakizorotesha nchi. © AP - Odelyn Joseph
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumanne Kenya ilitangaza kwamba itasitisha mpango wa kutuma maafisa wa polisi nchini Haiti siku moja baada ya kujiuzulu kwa Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry. Marekani ilijibu mara moja, ikisema haioni sababu ya kuchelewesha mpango huo.

Siku ya Jumatano, Rais wa Kenya William Ruto amesema alizungumza na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony Blinken kuhusu matukio ya hivi punde na akasisitiza dhamira ya Kenya ya kutekeleza ujumbe unaoungwa mkono na Umoja wa Mataifa katika nchi hiyo maskini ya Caribbean iliyokumbwa na mzozo wa kiusalama, kisiasa na kibinadamu.

Bw. Blinken "amenijulisha kwamba baraza jipya la rais litaundwa hivi karibuni ili kudhibiti hali nchini Haiti," Bw. Ruto alisema kwenye mtandao wa kijamii. "Nilimhakikishia Bw. Blinken kwamba Kenya itaongoza (katika misheni ya kimataifa) punde tu baraza la rais litakapoundwa," amesema.

Vyama vya kisiasa na shakhsia nchini Haiti vinajitahidi Jumatano kukubaliana juu ya muundo wa mamlaka ya mpito, katika jaribio la kurejesha hali ya utulivu katika nchi iliyodhoofishwa na magenge. Ariel Henry, aliyeteuliwa siku chache kabla ya mauaji  ya rais Jovenel Moïse mwaka 2021, alipingwa vikali katika miezi ya hivi karibuni. Aliamua kujiuzulu kufuatia shinikizo kutoka kwa magenge yenye silaha.

Jumatatu, wakati wa mkutano wa dharura na wawakilishi wa Haiti nchini Jamaika, Jumuiya ya nchi za Caribbean (Caricom), Umoja wa Mataifa na nchi kadhaa kama vile Marekani na Ufaransa zilitoa jukumu la kuunda "baraza la mpito la rais."

Nchini Kenya, kutumwa kwa maafisa wa polisi wa Kenya elfu moja kwenda Haiti kulikumbana na vikwazo vingi vya kisheria. Rais wa Kenya na Ariel Henry, hata hivyo, walitia saini makubaliano mnamo Machi 1 huko Nairobi kutuma maafisa wa polisi wa Kenya. Umoja wa Mataifa uliidhinisha mwezi Oktoba kutumwa kwa kikosi hiki, ambacho pia kinaungwa mkono na Marekani.

Mwishoni mwa mwezi wa Februari, nchi tano, ikiwa ni pamoja na Benin yenye zaidi ya wanajeshi 1,500, ziliarifu Umoja wa Mataifa kuhusu ushiriki wao katika misheni ya baadaye. Wanachama wengine wa ujumbe huu ni Bahamas, Bangladesh, Barbados na Chad, kwa mujibu wa msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Stéphane Dujarric.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.