DRC: Tanzania yatetea hatua ya kushiriki kwenye kikosi cha SADC
Nairobi – Tanzania imetetea hatua ya kushiriki kwenye kikosi cha kijeshi kutoka nchi za Jumuiya ya Kusini mwa Afrika SADC, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, ikisema inaunga mkono jitihada za kikanda chini ya mikataba ya Nairobi na Luanda ili kurejesha usalama katika eneo hilo.
Imechapishwa:
Waziri wa Mambo ya nje, January Makamba, ametoa ufafanuzi huo, baada ya madai kuwa wanajeshi wake wameendelea kurusha mabomu kuwalenga raia, katika operesheni ya kupambana na waasi wa M 23.
Makamba amesisitiza kuwa Tanzania, haishiriki kwenye operesheni hiyo peke yake bali, ipo kwenye kikosi cha SADC na inaunga mkono mikataba ya kikanda kurejesha amani jimboni Kivu Kaskazini.
Siku chache zilizopita, kundi la M23 lilitoa taarifa kulalamikia jeshi la Tanzania kuwalenga raia, kwenye maeneo wanayodhibiti na kuapa kujilinda.
Wakati hayo yakijiri, wiki hii kumeshuhudiwa mapigano makali kati ya jeshi la DRC na waasi wa M 23, huku kukiwa na ripoti kuwa waasi hao walikuwa mjini Sake, umbali wa Kilomita 25 kutoka mjini mkuu wa Kivu Kaskazini Goma.
Waziri wa Ulinzi,Jean Pierre Bemba, jana alitembelea Goma, na kuwahakikishia wakaazi wa mji huo serikali jijini Kinshasa itahakikisha kuwa wanalindwa dhidi ya hatari yoyote kutoka kwa waasi wa M 23.