Pata taarifa kuu

Uganda: Bobi Wine amethibitisha kuzuiliwa nyumbani kwake

Nairobi – Kiongozi wa upinzani nchini Uganda na aliyekuwa mgombea urais Bobi Wine, anasema anazuiliwa nyumbani kwake baada ya maofisa wa poliisi kuzingira makaazi yake kuelekea maandamano yaliyopangwa kufanyika.

Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi
Mwanasiasa wa upinzani nchini Uganda Robert Kyagulanyi AFP - YASUYOSHI CHIBA
Matangazo ya kibiashara

Wanasiasa wa upinzani walikuwa wamepanga maandamano siku ya Alhamisi kupinga ubovu wa barabara nchini Uganda, nchi hiyo ikitarajiwa kuwa mwenyeji wa mikutano miwili mikubwa ya kimataifa.

Kwa mujibu wa Wine, polisi na wanajeshi wamemzuia kuondoka nyumbani kwake Magere, kaskazini mwa mji mkuu Kampala.

Kupitia ujumbe kwenye ukurasa wa X, mwanamuziki huyo wa zamani amesema kuwa "Wanajeshi waoga na polisi wamezingira nyumba yetu na kutuweka chini ya kizuizi cha nyumbani, lakini maandamano yanaendelea."

Wine, ambaye jina lake halisi ni Robert Kyagulanyi, aliwania dhidi ya rais Yoweri Museveni katika uchaguzi uliopita wa mwaka 2021 na amekuwa na kauli kuwa anataka ukomeshwe utawala wa mkono wa chuma chini ya Museveni.

Aliyekuwa mgombea urais Kizza Besigye wa chama cha upinzani cha Forum for Democratic Change naye pia amethibitisha kwamba yeye pia hakuruhusiwa kuondoka nyumbani kwake.

"Tumezuiliwa nyumbani na WAOGA! Hakuna kurudi nyuma, tunastahili mambo mema. Tafadhali fanya uwezavyo, popote ulipo, kwa chochote ulicho nacho, ili kuonyesha barabara mbaya zinazokuathiri leo," alichapisha kwenye X.

Msemaji wa polisi Patrick Onyango amethibitisha kutumwa kwa walinda usalama nje ya makaazi ya wanasiasa hao wawili akisema kuwa wamechukua hatua hiyo kuwazuia kufanya maandamano yasiokuwa na idhini.

Vyama vya upinzani vimeishutumu serikali kwa kuwakamata watu wasio na makazi na kuharibu maelfu ya vibanda vilivyo kando ya barabara katika harakati za kufanya usafi kabla ya mkutano wa jumuiya ya nchi zisizoegemea upande wowote na G77 mjini Kampala.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.