Pata taarifa kuu

Raia wa DRC wajiandaa kupiga kura siku ya Jumatano

Siku ya Jumatano, takriban wapiga kura milioni 44 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, wanajiandaa kupiga kura kumchagua rais, wabunge wa kitaifa, wale wa Mikoa na madiwani wa Manispaa mbalimbali.

Vifaa vya kupigia kura, mwaka 2018
Vifaa vya kupigia kura, mwaka 2018 John WESSELS / AFP
Matangazo ya kibiashara

Licha ya changamoto ya usambazaji wa vifaa vya kupigia kura, Tume ya Uchaguzi CENI, inasema raia wa DRC watapiga kura kama ilivyopangwa, Desemba, 20.

Saa chache kabla ya vituo vya kupigia kura kufunguliwa, msemaji wa CENI Patrice Nseya Mulela, amesema vifaa vya kupigia kura vinasafirishwa kwenda katika vituo mbalimbali mkoani Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri, kwa msaada wa jeshi la kulinda amani MONUSCO.

Mshindi atapatikana vipi ?

Matokeo ya awali, yanatarajiwa kutangazwa tarehe 31 mwezi Desemba, lakini Tume ya Uchaguzi inaweza kutangaza mapema iwapo zoezi la kuhesabu na kujumuisha matokeo litakuwa limekamilika.

Mgombea yeyote atakayepata kura nyingi, atatangazwa mshindi. Hakuna duru ya pili na sio lazima mshindi kupata asilimia 50 ya kura.

Mshindi atakuwa madarakani kwa kipindi cha miaka mitano, lakini anaweza kuwania tena kwa muhula wa pili na wa mwisho.

Mambo muhimu kuhusu uchaguzi huu

Kuna wagombea zaidi ya 20, wanaotafuta uongozi wa nchi hiyo, akiwemo rais Felix Tshisekedi, anayetafuta muhula wa pili.

Tshisekedi anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa Moise Katumbi, mfanya biashara tajiri na Gavana wa zamani wa jimbo la Katanga.

Mwingine ni mgombea wa mwaka 2018, Martin Fayulu, anayeaminiwa kushinda uchaguzi uliopita, lakini pia Daktari wa magonjwa ya wanawake na mshindi wa tuzo ya Nobel Denis Mukwege.

Historia zaidi

Nchi ya pili kwa ukubwa barani Afrika yenye utajiri mkubwa wa madini kama shaba, dhahabu, Coltan na Cobalt lakini wananchi wake wengi ni masikini.

Ina ukubwa wa Kilomita za mraba Milioni 2.34, sawa na Ulaya Magharibi.

Ina watu wanaokaridiwa kuwa Milioni 100, kutoka makabila 250. Mikoa ya Mashariki, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini na Ituri kwa kipindi kirefu imeendelea kukabiliwa na utovu wa usalama kutokana na kuwepo kwa makundi mengi ya waasi.

Kifaransa ndio lugha rasmi. Hata hivyo, lugha zingine zinazozunguzwa ni pamoja na Kikongo, Lingala, Tshiluba na Kiswahili, zinatambuliwa kama lugha za taifa.

Serikali mbili, ziliwahi kuondolewa madarakani na jeshi mwaka 1965 na 1997.

Viongozi wake wawili waliuawa wakiwa madarakani. Patrice Lumumba mwaka 1961 na Laurent-Desire Kabila mwaka 2001.

Mwaka 2018, ilikuwa mara ya kwanza kwa DRC kushuhudia makabidhiano ya madaraka kwa amani, baada ya Felix Tshisekedi kuapishwa na kuchukua hatamu za uongozi kutoka kwa mtangulizi wake Joseph Kabila, baada ya uchaguzi wa urais ambao, hata hivyo kulikuwa na madai ya wizi wa kura.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.