Pata taarifa kuu

Mashirika ya misaada yaonya kupungua kwa ufadhili nchini DRC

Mashirika ya kibinadamu yanaonya kuhusu kuendelea kuzorota kwa hali ya kibinadamu Mashariki mwa nchi ya Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wakati huu kupungua kwa ufadhili kumesababisha mashirika hayo kushindwa kufikia lengo.

Mama akiwa na mtoto wake wakati wafanyakazi wa shirika la NRC walipotembelea kambi ya Kahe, jirani na Rutshuru, Kivu Kaskazini. 21.08.2023
Mama akiwa na mtoto wake wakati wafanyakazi wa shirika la NRC walipotembelea kambi ya Kahe, jirani na Rutshuru, Kivu Kaskazini. 21.08.2023 © NRC
Matangazo ya kibiashara

Mashirika hayo likiwemo shirika la kimataifa la mpango wa chakula WFP na lile la Norway la baraza la wakimbizi, NRC, kupungua kwa ufadhili huenda hivi karibuni kukawafanya washindwe kuwasaidia mamilioni ya raia wa Kongo wanaokabiliwa na njaa na kukosa huduma muhimu.

Kwa mujibu wa baraza la wakimbizi la Norway, miezi ya hivi karibuni kumeshuhudiwa kuzorota kwa hali ya kibinadamu mashariki mwa DRC, ambako raia wameendelea kushambuliwa huku wahusika wakiwa hawajashughulikiwa.

"Kutotazamwa kwa karibu ambapo mamia ya raia wanataabika mashariki mwa Kongo ni jambi lisilosameheka, ni janga kubwa kubwa zaidi la njaa duniani. Watu milioni 25 wameachwa peke yao, wanakabiliwa na magonjwa na mashambulio."  Amesema Jan Egeland, katibu mkuu wa baraza la wakimbizi nchini Norway.

Kwa mujibu wa Egeland, miezi 8 ya mwaka huu 2023, chini ya robo ya ufadhili uliohitajika kutoa misaada ya kibinadamu nchini DRC umepokelewa.

"Ni jambo lisilokubalika kwamba mashirika ya misaada yanalazimika kuchukua hatua ngumu kuamua nani asaidiwe na nani asisaidiwe, haikubaliki kwamba mataifa mengi tajiri, mashirika na watu wanakataa kutoa kiwango fulani cha mchango kwa mamilioni ya raia wanaotaabika,” alisema Egeland.

Katika mahojiano ya kipekee aliyoyafanya na idhaa ya RFI Kiswahili akiwa ziarani mashariki wa DRC, Egeland, ametoa wito kwa serikali ya Kinshasa kuhakikisha inawalinda raia Wake.

00:37

Jan Egeland - Katibu mkuu wa Shirika la Baraza la Wakimbi la Norway

“Ujumbe wetu ni kwamba, serikali inahitaji kufanya zaidi kuwalinda raia, kuzuia vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na hasa ukatili wa kijinsia. Lazima ifanye zaidi kuleta maridhiano baina ya makabila na jamii nyingine. Na sisi tunaahidi kuendelea kufanya juhudi kuwaleta tena wafadhili katika taifa hili ambalo mahitaji yanaongezeka na misaada ya kibinadamu inapungua,” aliongeza Egeland.

 

Mtoto akiwa amembeba mdogo wake katika kambi ya Kahe, Rutshuru mashariki mwa DRC. 21 August 23
Mtoto akiwa amembeba mdogo wake katika kambi ya Kahe, Rutshuru mashariki mwa DRC. 21 August 23 © ©NRC

Aidha katika tarifa yake kwa vyombo vya habari, NRC imesema mashambulio na mauaji ya hivi karibuni yamesababisha hali ya dharura kwa mzozo ambao tayari ulisahaulika.

 

NRC imeongeza kuwa, Jumuiya ya Kimataifa lazima isaidie kuhakikisha inatoa misaada itakayoendana na hali ilivyo kwenye jimbo la Ituri na êneo zima la mashariki mwa nchi hiyo.

Shirika hilo linadai kuwa machafuko ya makundi ya waasi kwenye jimbo la Ituri, yamesababisha watu zaidi ya laki 5 kukumbia nyumba zao katika miezi ya hivi karibuni, ikichangia watu milioni 1 na laki 7 ambao walilazimika kukimbia machafuko.

Egeland kwenye taarifa yake amesema pia, watoto laki 7 na elfu 50 wamelazimika kuacha masomo kutokana na vurugu zinazoendelea kwenye jimbo la Ituri pekee.

“Pale ambapo watoto wanakosa haki ya kupata elimu, kasi ya vitendo vya udhalilishaji wa kingono inaongezeka, utumwa, ndoa za mapema na kusajiliwa kwenye makundi ya wapiganaji.” Amesema Egeland.

 

Maeneo mengi ya shule yanakaliwa. Hapa ni Rutshuru.  21 August 23
Maeneo mengi ya shule yanakaliwa. Hapa ni Rutshuru. 21 August 23 © NRC

Ushahidi na Takwimu:

  • DRC ni miongoni mwa nchi zinazokabiliwa na janga la njaa duniani, watu milioni 25 wakihangaika kila siku kupata chakula cha kutosha. (WFP)
  • Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ni mwenyeji wa mojawapo ya idadi kubwa zaidi ya watu waliokimbia makazi yao duniani na imeorodheshwa kama mojawapo ya janga la uhamishaji lililopuuzwa zaidi ulimwenguni kwa miaka saba iliyopita, kulingana na ripoti ya kila mwaka ya NRC.
  • DRC inahifadhi mojawapo ya idadi kubwa ya watu waliokimbia makazi yao (ikiwa ni pamoja na wakimbizi) - takriban milioni 5.5. Wengi wako mashariki mwa nchi. (UNHCR)
  • Fedha kidogo zinazotolewa kwa ajili ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo hutoka kwa kikundi kidogo sana cha wachangiaji: zaidi ya 80% ya msaada wa sasa wa kifedha unatoka kwa wafadhili 5 pekee (UNOCHA)
  • Katika kipindi cha miezi minane ya kwanza ya mwaka huu, ni theluthi moja tu ya fedha muhimu kwa DRC imetengwa. Kwa jinsi hali ilivyo, DRC inakosa takriban 70% ya kile inachohitaji katika misaada. (UNHCR)
  • Sekta ya elimu imeathiriwa zaidi na janga hili, ambapo mtoto 1 kati ya 3 hawakuwa shuleni mwanzoni mwa 2022, na zaidi ya shule 230 zimefungwa. (UNICEF)
  • Mwanamke mmoja kati ya saba alikumbana na ukatili wa kingono kabla ya kufikia umri wa miaka 18, na tatizo ni kubwa zaidi katika jamii zilizoathiriwa na migogoro. (NRC)
  • Migogoro mingi ya kibinadamu inakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha. Kwa kila dola ya misaada ya kibinadamu iliyopatikana kwa kila mtu anayehitaji nchini Ukraine, kwa mfano, senti 25 pekee ziliongezwa kwa kila mtu aliyehitaji katika majanga 10 yaliyopuuzwa zaidi duniani. (NRC)
  • Mnamo 2022, idadi ya watu wanaohitaji msaada nchini DRC ilikuwa kubwa zaidi kuliko idadi ya watu wanaohitaji nchini Ukrainia, lakini kiasi cha ufadhili kilichopatikana kilikuwa chini kwa 74%.
Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.