Raia wa Rwanda ni wafungwa nchini mwao: Rusesabagina
Nairobi – Mkosoaji wa serikali ya Rwanda Paul Rusesabagina, ambaye alijipatia umaarufu kwa juhudi zake za kuwaokoa watu wakati wa mauaji ya kimbari ya mwaka wa 1994, amedai kuwa raia wa Rwanda ni wafungwa katika nchi yao.
Imechapishwa:
Katika ujumbe wake wa kwanza hadharani tangu kuachiwa huru kutoka jela nchini Rwanda mwezi Machi baada ya zaidi ya siku 900 gerezani, Rusesabagina aliishukuru Marekani kwa kuongoza mchakato wa kuachiwa kwake kutoka katika kile alichokitaja kama "kuzimu".
Aidha ameeleza kuwa ujumbe wake wa video kwenye mtandao wa YouTube ulitolewa ili kuendana na tangazo la uhuru wa Rwanda Julai 1, 1962.
"Kwa bahati mbaya leo, miaka 61 baadaye, Wanyarwanda bado hawapo huru. Wanyarwanda ni wafungwa ndani ya nchi yao," alisema Rusesabagina, akizungumza kutoka nyumbani kwake San Antonio katika jimbo la Texas nchini Marekani.
"Rwanda ni serikali ya kimabavu ambayo haina haki kwa raia wake na haivumilii upinzani kwa raia wake."
Rusesabagina aliachiliwa huru mwezi Machi 25 baada ya zaidi ya siku 939 gerezani, baada ya serikali ya Kigali kubatilisha kifungo chake cha miaka 25 kwa tuhuma za ugaidi.
"Nataka kushukuru serikali ya Marekani kwa kuingilia kati na kushughulikia kesi yangu," alisema.
Kuzuiliwa kwa Rusesabagina mwenye umri wa miaka 69, kuliibua suala la kuwa Rwanda inahusika na ukandamizaji wa wapinzani wa kisiasa na uhuru wa kujieleza chini ya utawala wa rais Paul Kagame, ambaye Rusesabagina amekuwa akimtaja kama "dikteta".
Washington imesema Rusesabagina "alizuiliwa kimakosa" baada ya ndege iliyombeba kwenda Burundi kuelekezwa Rwanda mnamo Agosti 2020.
Rusesabagina, anasifiwa kwa kusaidia kuokoa maisha ya takriban 1,200 wakati wa mauaji ya halaiki ya 1994 ambapo takriban watu 800,000 waliuawa, hasa Watutsi lakini pia Wahutu wenye msimamo wa wastani.