Pata taarifa kuu

Uganda: Wabunge wapitisha rasimu mpya ya sheria dhidi ya ushoga

NAIROBI – Bunge la Uganda Jumanne, Mei 2, limepitisha rasimu mpya kuhusu sheria dhidi ya mashoga nchini humo, ambapo wabunge wameunga mkono vifungu vingi vilivyokuwa katika ile rasimu ya kwanza.

Bunge la Uganda wakati wa kikao hicho limeidhinisha sheria inayoimarisha adhabu ya ndoa za jinsia moja.
Bunge la Uganda wakati wa kikao hicho limeidhinisha sheria inayoimarisha adhabu ya ndoa za jinsia moja. REUTERS - ABUBAKER LUBOWA
Matangazo ya kibiashara

Spika wa bunge Annet Anita Among, amesema mswada huo umepitishwa baada ya wabunge kuupigia kura, mbunge mmoja tu ndio alipiga kura ya hapana.

Tuna utamaduni ambao tunapaswa kulinda. Mataifa ya magharibi hayawezi kuja kututawala hapa Uganda, Amesema Among.

Wabunge walifanyia marekebisho sehemu ya rasimu ya sheria hiyo, ili kufafanua kuwa kujitambulisha kama shoga hakutakuwa kosa la jinai, lakini kujihusisha na vitendo vya ushoga, litakuwa ni kosa linaloadhibiwa kwa kifungo cha maisha jela.

Mwezi Aprili, rais Yoweri Museveni alikutana na wabunge na kuwashauri kurejelea baadhi ya vipengee, na sasa baada ya kupitishwa inamaanisha kuwa watu wanaorudia makosa ya ushoga wanaweza kuhukumiwa kifo.

Vifungu vilivyobadilishwa

Rasimu ya awali ilikuwa ikiwataka raia wa Uganda kuripoti tukio lolote la ushoga kwa polisi, la sivyo angehukumiwa miezi sita jela.

Wabunge hivi leo wameamua kufanyia marekebisho kifungu hicho baada ya Museveni kusema kipengee hicho kinatishia kuleta mgogoro katika jamii.

Badala yake, hitaji la kuripoti sasa linahusu tu tuhuma za makosa ya kingono dhidi ya watoto na watu walio katika mazingira magumu, huku adhabu ikiongezwa hadi miaka mitano jela.

Mswada huo sasa utatumwa kwa rais Museveni, ambaye anaweza tena kuchagua kutumia kura yake ya turufu au kutia saini kuwa sheria.

Rais wa Uganda, Yoweri Museveni
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni © StateHouseUganda

 

Iwapo mswada huu utarejeshwa bungeni kwa mara ya tatu, wengi wa wabunge wanaweza kubatilisha kura yake ya turufu, na kulazimisha mswada huo kupita, kwa sababu sheria hiyo inaungwa mkono na umma nchini Uganda na uhuru wa kujieleza wa mashirika ya kiraia nchini humo umeminywa.

Mswada wapingwa kimataifa

Mwezi uliopita, bunge la Ulaya lilipiga kura kulaani mswada huo na kuzitaka nchi wanachama, kumshawishi Museveni kutotia saini mswada huo na kuwa sheria, likionya kuwa uhusiano na Kampala utakuwa hatarani.

Ikulu ya Marekani pia imeonya serikali ya Uganda kuhusu uwezekano wa athari za kiuchumi ikiwa sheria hiyo itaanza kutumika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.