Pata taarifa kuu

Mkanyagano mbaya nchini Uganda: washtakiwa wawili waachiliwa kwa dhamana

Watu wawili walioshtakiwa katika uchunguzi kuhusu mkanyagano ulioua watu 10 usiku wa kuamkia mwaka mpya nchini Uganda wameachiliwa kwa dhamana, mahakama imetangaza siku ya Jumanne Janauri 10, 2023.

Maafisa wa Polisi wa Uganda mjini Kampala.
Maafisa wa Polisi wa Uganda mjini Kampala. © Nicholas Bamulanzeki/AP
Matangazo ya kibiashara

Waathiriwa wa mkanyagano, wengi wao wakiwa na umri wa kati ya miaka 10 na 20, walikuwa miongoni mwa umati uliojaa kwenye njia ndogo kutazama fataki zikipigwa nje ya kituo cha ununuzi cha Freedom City kusini mwa mji mkuu wa Kampala.

Watazamaji walikuwa na sehemu moja tu ya kuingia na kutoka. Waandalizi walikuwa wamezuia viingilio vingine ili kuzuia watu ambao hawajalipa wasijipenyeze.

Mwandaaji wa sherehe za mkesha wa mwaka mpya Abby Musinguzi, anayejulikana kwa jina la Abitex na mwenzake Elvis Francis Juuko wanashitakiwa kwa makosa 13 yakiwemo ya uzembe na kusababisha vifo na majeraha.

Mahakama mjini Kampala imewapa washtakiwa hao wawili dhamana baada ya kulipa kiasi cha shilingi milioni mbili, takriban euro 540. Chumba cha mahakama kilikua kimejaa manusura, jamaa za waathiriwa pamoja na familia za washtakiwa wawili, wanasiasa na mawakili.

Abby Musinguzi na Elvis Francis Juuko watasikilizwa tena na mahakama katika kikao cha mahakama Februari 7, wakili wao, Erias Lukwago, ameiambia shirika la habari la AFP. Elvis Francis Juuko alikamatwa Ijumaa katika mtaa wa Mityana, kilomita 60 kutoka Kampala, alikokuwa amejificha, kwa mujibu wa polisi.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni aliagiza uchunguzi wa haraka ufanyike kuhusu mkasa huo na kuzipa familia za marehemu shilingi milioni 5 za Uganda, karibu euro 1,340, kwa ajili ya gharama za mazishi.

Sherehe hizi za Mwaka Mpya nchini Uganda, nchi ya Afrika Mashariki, zilikuwa za kwanza katika kipindi cha miaka mitatu, baada ya vikwazo kutokana na janga la UVIKO-19 na matatizo ya usalama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.