ICC: Kesi dhidi ya mfanyabiashara Félicien Kabuga kuanza Septemba 29 Hague
Kesi dhidi ya mfanyabiashara na mshukiwa wa mauaji ya kimbari nchini Rwanda Félicien Kabuga, sasa itaanza tarehe 29 mwezi Septemba kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC jijini Hague.
Imechapishwa:
Uamuzi huo, umefikiwa na Majaji wa Mahakama hiyo, baada ya Kabuga mwenye umri wa miaka 87 kufika mbele yao kusikiliza utaratibu wa namna kesi yake itakavyoendeshwa.
Kabuga,alikamatwa na kuzuiwa nchini Ufaransa mwaka uliopita, baada ya kukwepa kukamatwa kwa zaidi ya miaka 20. Aidha, Majaji wameamua kuwa, kwa sababu ya hali yake ya kiafya ataruhusiwa kuhudhuria vikao hivyo kwa njia ya vídeo kama italazimika kufanya hivyo.
Wakati akiwa nchini Rwanda, alikuwa rais wa kituo cha redio na Televisheni Libre des Mille Collines, ambazo zilitumiwa kutangaza kuuawa kwa Watutsi wakati wa mauaji ya kimbari mwaka 1994.
Anatuhumiwa kuhusika kupanga mauaji ya kimbari, uchochezi yaliyosababisha mauaji hayo na uhalifu dhidi ya binadamu.
Mauaji ya kimbari nchini Rwanda, yalisababisha vifo vya watu 800,000, wengi wakiwa Watutsi.