Pata taarifa kuu

Rais wa Tanzania John Magufuli, afariki dunia

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, amefariki dunia Jumatano ya wiki hii akiwa na umri wa miaka 61, baada ya kuugua kwa muda mfupi kutokana na maradhi ya moyo aliyokuwa akisumbuliwa kwa zaidi ya miaka 10.

Picha ya Maktaba ikimuonesha Marehemu raliyekuwa rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, katika moja ya mikutano ya chama chake.
Picha ya Maktaba ikimuonesha Marehemu raliyekuwa rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli, katika moja ya mikutano ya chama chake. AP
Matangazo ya kibiashara

Akihutubia taifa kupitia TBC, makamu wa rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, amesema rais Magufuli, alifariki maajira ya saa kumi na mbili jioni katika hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam.

Makamu wa rais, amesema rais Magufuli alilazwa tarehe 6 ya mwezi Machi katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kwa tatizo la mfumo wa umeme wa moyo, ambapo tarehe 7 aliruhusiwa kutoka hospitali.

Makamu wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan
Makamu wa rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan www.unmict.org
Mheshimiwa rais Magufuli, alilazwa tarehe 6 Machi katika taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete kwa tatizo la moyo la mfumo wa umeme, ambalo alikuwa nalo kwa zaidi ya miaka 10, alituhusiwa tarehe 7 machi mwaka huu na kuendelea na majukumu yake.
Tarehe 14 Machi mwaka huu alijisikia vibaya na akakimbizwa hospitali ya Mzena ambapo aliendelea na matibabu chini ya uangalizi wa madaktari na wauguzi wa taasisi ya moyo ya Jakaya Kikwete hadi umauti ulipomkuta.

Aidha makamu wa rais Samia Suluhu Hassan, amesema tayari mipango ya mazishi imeanza ambapo wananchi watajulishwa ambapo pia ametangaza nchi kuwa katika kipindi cha maombolezo kwa siku 14 na bendera kupepea nusu mlingoti.

Kifo cha Magufuli kimetangazwa baada ya majuma kadhaa za uwepo wa taarifa za kuugua kwake kupitia mitandao ya kijamii, ambapo hata baadhi walidiriki kudai alikwishafariki, taarifa ambazo hata hivyo zilikanushwa na Serikali.

Ni juma hili tu pia, ambapo makamu wa rais Samia Suluhu Hassan, akiwa ziarani mkoani Tanga, aliwataka wananchi kuwa watulivu na kushikamana hasa wakati huu ambapo amesema nchi inapitia kipindi kigumu cha vita ya uchumi.

Kifo chake kimeelezwa na wadadisi wengie wa masuala ya siasa kama pigo kwa Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla, kutokana na uongozi wake tanguj alipoingia madarakani kwa mara ya kwanza mwaka 2015, ambapo alijipatia umaarufu ndani na nje ya nchi na kupeza hata jina la utani kama ''Buldozer''.

Atakumbukwa punde tu baada ya kuingia madarakani, alitangaza kuahirishwa kwa sherehe wa uhuru na kuagiza fedha za maandalizi ya sherehe hizo kutumiwa kujenga barabara na miundombinu mingine.

Magufuli pia alifahamika sana kwa kuchukua hatua za papo kwa papo kwa viongozi alioamini walishindwa kutimiza majukumu yao ambapo mawaziri na wafanyakazi kadhaa walifutwa kazi.

Miongoni mwa masuala mengine aliyojizolea umaarufu ni pamoja na kuagiza uhakiki wa vyeti kwa waanyakazi wa uma ambapo maelfu ya wafanyakazi walifutwa kazi.

Rais Magufuli pia atakumbukwa kwa misimamo yake ya kutetea haki za wanyonge na jumuiya ya Afrika Mashariki, ambapo alikuwa na usemi maarufu wa ''Hapa Kazi Tu''.

Rais Magufuli pia alikuwa mfano kwa viongozi kadhaa wa Afrika ambapo baadhi hata waliiga namna ya utendaji kazi wake, ambaoo atakumbukwa kwa kuzuia safari za nje kwa viongozi wa uma.

Hata hivyo licha ya mafanikio makubwa ya utawala wake, rais Magufuli pia alikuwa akikosolewa kwa masuala kadhaa ikiwemo Serikali yake kukithiri kwa vitendo vya ukiukwaji wa haki wa binadamu na kujaribu kuminya uhuru wa vyombo vya habari.

Suala jingine alilojikuta katika shinikizo ni namna nchi yake ilivyoshughulikia janga la virusi vya Corona, ambapo alitangaza taifa hilo kuwa huru na virusi hivyo katikati ya mwaka jana, kabla ya mwezi mmoja uliopita, kukiri kuwepo tena kwa wimbi la pili la maambukizi.

Rais Magufuli alizaliwa katika kijiji cha Chato, tarehe 29 ya mwezi Octoba mwaka 1959.

Alichaguliwa kwa mara ya kwanza kama mbunge mwaka 1995, ambapo alihudumu kama naibu waziri wa ujenzi kati ya mwaka 1995 hadi 2000.

Mwaka 2000 hadi 2006 alikuwa waziri wa ujenzi, kabla ya kuteuliwa juwa waziri ardhi na makazi kuanzia mwaka 2006 hadi 2008.

Mwaka 2008 hadi 2010 alihudumu kama waziri wa mifugo na uvuvi na baadae kuwa tena waziri wa ujenzi kati ya mwaka 2010 hadi 2015 ambapo alichaguliwa na chama tawala nchini Tanzania CCM kuwa mgombea wake wa kiti cha urais.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.