Pata taarifa kuu
MAREKANI-PAKISTANI

Marekani yasema shambulio dhidi ya Osama Bin Laden halikuwa la mauaji

Serikali ya Marekani imesema Shambulio la Makomandoo wa nchi hiyo la kumuua Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Duniani Osama Bin Laden halikuwa la mauaji bali lilikuwa na lengo la kumkamata akiwa hai au kumuua iwapo watashindwa kumtia nguvuni akiwa hai.

Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Duniani Osama Bin Laden akizungumza kwenye mkutano wa waandishi mnamo mwake 1998
Kiongozi wa Mtandao wa Al Qaeda Duniani Osama Bin Laden akizungumza kwenye mkutano wa waandishi mnamo mwake 1998 @Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Marekani Eric Holder ndiye ambaye ametoa kauli hiyo na kusema usalama wa Makomandoo hao wa Nchi Kavu ulikuwa muhimu zaidi na ndiyo maana wakaamua kumpiga risasi na kumuua Osama baada ya kumkamata.

Holder amenukuliwa katika mahuajiano na chombo kimoja cha habari akisema hatua ambayo ilichukuliwa ya kumuua Osama ilikuwa ni kwa ajili ya kulilinda taifa hilo kitu ambacho kimekuwa kikifanyika mara nyingi.

Mwanasheria huyo amesisitiza shambulio hilo lilikuwa na lango la kumuua au kumkamata lakini usalama wa vikosi na taifa la Marekani uliwekwa mbele na ndiyo maana wakaamua kumuua Osama baada ya kumkamata kwenye jumba lake.

Holder ameongeza kuwa baada ya Makomandoo kumfikia Osama kulikuwa na kila dalili za yeye kuweza kujilipua kabla ya kushikwa na ndiyo maana uamuzi wa kumpiga risasi ukachukuliwa.

Mwanasheria huyo anaongeza kuwa Osama Bin Laden alijiapiza kuwa hawezi kukamatwa akiwa hai kitu ambacho kiliongeza hofu kwa Makomandoo hao na kuamua kumuua kama njia mbadala ya kutekeleza operesheni hiyo.

Ufafanuzi juu ya shambulio hilo unakuja baada ya Mtoto wa Osama Bin Laden kunukuliwa akihoji ni kwa nini baba yake alipigwa risasi badala ya kukamatwa na kupelekwa mbele ya vyombo vya sheria ili ukweli uweze kubainika kwa dunia.

Mapema siku ya jumanne Mtoto wa Osama amesema mauaji ya baba yake yalikuwa yamepangwa na kukanusha kuzikwa baharini kama ambavyo serikali ya Marekani ilivyoutangazia ulimwengu.

Osama Bin Laden aliuawa katika Mji wa Abbottabad nchini Pakistani akiwa katika nyumba ambayo anakisiwa kuishi kwa kipindi cha miaka mitano ikiwa karibu na Kambi ya Jeshi ya nchi hiyo.

Tangu Osama auawe na Makomandoo wa Marekani tarehe 2 ya mwezi May kumekuwa na kauli zinazokinzana juu ya kifo chake na hata mahali alipozikwa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.