Mvua kubwa yasababisha maafa Beijing, China
Nairobi – Karibia watu 11 wamefariki wakati wengine 27 hawajulikani waliko baada ya mvua kubwa inayoendelea kunyesha jijini Beijing nchini China kusababisha mafuriko na uharibifu wa miundo mbinu.
Imechapishwa:
Miongoni mwa watu waliofariki ni wafanyikazi wawili wa uokoaji walioangamia wakati wakiwa kazini kutoa huduma za msaada.
Zaidi ya watu laki moja kwenye jiji hilo ambao walikuwa wanakabiliwa na hatari ya kuathiriwa na mafuriko wamehamishwa katika maeneo salama.
Baadhi ya barabara zimeonekana kuharibiwa na mafuriko yaliosababishwa na mvua hiyo wakati huu maofisa wa uokoaji wakiendelea na shughuli za kuwatafuta watu wanaohofiwa kuwa huenda wamefunikwa na udongo.
Rais wa China Xi Jinping, ametoa wito wa kufanyika kwa "kila juhudi" kuokoa watu "walionaswa" kwenye matope baada ya mvua kubwa kunyesha katika maeneo ya kaskazini mwa nchi, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.
Mamlaka za mitaa "lazima zifanye kazi nzuri katika kutibu waliojeruhiwa na kufariji familia za wahasiriwa, na kupunguza majeruhi", CCTV ilimnukuu Xi akisema.
Picha za moja kwa moja kutoka kwa kituo cha utangazaji cha CCTV Jumanne asubuhi zilionyesha baadhi ya mabasi yakiwa yamezama kwenye maji ya mafuriko katika kitongoji cha Beijing kusini magharibi mwa Fangshan.