Watu 22 wamefariki katika mafuriko Korea kusini
Takriban watu 22 wamefariki na wengine 14 hawajulikani walipo baada ya mvua kubwa kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi nchini Korea Kusini wakati huu maelfu ya wengine wakitakiwa kuhama makazi yao.
Imechapishwa:
Mvua kubwa imekuwa ikinyesha nchini humo kwa kipindi cha siku tatu zilizopita, na kusababisha mafuriko na maporomoko ya ardhi hali ambayo imechangia kufurika kwa bwawa kubwa.
Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani nchini humo, watu 22 wameuawa na wengine 14 hawajulikani walipo kutokana mvua hiyo kubwa, wengi wao wakiwa wamezikwa na maporomoko ya ardhi wengine wakiripotiwa kuanguka kwenye bwawa lililofurika.
Shirika la habari la Yonhap la Korea Kusini lilikuwa limeripoti awali vifo 24, likiwanukuu maafisa wa shirika la kutoa misaada.
Zaidi ya wakaazi 6,400 katika kaunti ya kati ya Goesan wameombwa kuhama makazi yao baada ya bwawa la Goesan kuaanza kufurika.
Baadhi ya watu ambao wameripotiwa kutoweka walisombwa na maji wakati mto ulipofurika katika jimbo la Gyeongsang Kaskazini, wizara hiyo ilisema.
Idadi ya vifo inatarajiwa kuongezeka wakati mashirika ya serikali ya mitaa yanatathmini uharibifu huo kote nchini.