Pata taarifa kuu
UINGEREZA-IRAN-USHIRIKIANO-USALAMA

Uingereza yapendekeza jeshi la Ulaya katika Ghuba ya Uajemi, Iran yalaani

Uingereza inajiandaa kuzindua kikosi kitakachoongozwa na nchi za Ulaya kujibu hatua ya Iran ya kuikamata meli ya mafuta iliyokuwa na bendera ya Uingereza mnamo Julai 19, kwa mujibu wa vyanzo kutoka Uingereza.

Jeshi la Marekani likipiga doria kwenye pwani ya Hormuz, Desemba 21, 2018.
Jeshi la Marekani likipiga doria kwenye pwani ya Hormuz, Desemba 21, 2018. REUTERS/Hamad I Mohammed
Matangazo ya kibiashara

Ni wiki mbili sasa tangu kukamatwa meli ya Uingereza – ‘'Stena Impero'' ambapo hali hiyo imejitokeza baada ya kikosi cha wanamaji wa Uingereza kuitia nguvuni meli ya Iran ‘'Grace 1'' katika pwani ya Gibraltar kwa madai kwamba ilikuwa inasafirisha mafuta kwenda Syria hatua, ambayo inakiuka vikwazo vya Umoja wa Ulaya.

Siku ya Jumatatu wiki iliyopita Uingereza ilipendekeza kuwepo kwa jeshi la Ulaya katika Ghuba ya Uajemi, ili kukabiliana na chokochoko za Iran dhidi ya kile inachoda ni ”mahisimu wake”.

Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Annegret Kramp-Karrenbauer, amesema kuwa Ujerumani inaweza kushiriki katika kuundwa kikosi cha jeshi kilichopendekezwa na Uingereza. Naye Waziri wa Mambo ya nje wa nchi hiyo Heiko Maas amesema hata hivyo mipango hiyo bado ipo kwenye hatua za mwanzoni.

Hata hivyo Iran imelaani pendekezo la Uingereza la kuanzisha kikosi cha walinzi wa bahari wa Ulaya katika Ghuba ya Uajemi. Iran imesema hatua hiyo ni uchokozi.

Wakati huo huo Merikani imesema itaongeza uwepo wa majeshi yake katika eneo hilo ili kufuatilia shughuli za Iran. Lakini Iran imesema inaamini nchi za Mashariki ya Kati ndio zinapaswa kuhakikisha usalama wa meli zinazopita kwenye bahari ya Hormuz.

Rais wa Iran Hassan Rouhani amesema uwepo wa vikosi vya kigeni katika eneo hilo hautasaidia chochote bali hatua hiyo itasababisha mvutano. Rais Rouhani, ameongeza kusema kuwa Iran na Oman ndio zenye jukumu la msingi la kulinda eneo muhimu la pwani ya Hormuz.

Iran pia imesisitiza kuwa hali mbaya na mivutano ya sasa katika Mashariki ya Kati inatokana na kujiondoa kwa Marekani katika mpango wa nyuklia wa mwaka 2015 (JCPOA), uliofikiwa kati ya Iran na mataifa yenye nguvu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.