Korea Kaskazini yamtusi makamu wa rais wa Marekani
Nchi ya Korea Kaskazini imemjia juu makamu wa rais wa Marekani Mike Pence, ikimuita kiongozi huyo “mjinga na asiye na maarifa” wakati huu utawala wa Pyongyang ukitishia kujitoa kwenye mazungumzo kati ya nchi hizo mbili.
Imechapishwa:
Katika taarifa iliyotolewa naibu waziri wa mambo ya nje wa Korea Kaskazini Choe Son Hui, amesema matamshi ya Pence ya hivi karibuni hayakupaswa kutolewa na kwamba kama haitaki mazungumzo nchi yao iko tayari kurejelea mpango wake wa nyuklia.
Korea Kaskazini imesema itafikiria tena iwapo itahudhuria mkutano ikiwa Marekani itaendelea kusisitiza kuwa iachane na mpango wa silaha za nyuklia.
Hata hivyo waziri wa mambo ya nje wa Marekani Mike Pompeo ametupilia mbali uwezekano wa kutofanyika kwa mazungumzo hayo, akisema mwenye usemi wa mwisho ni Kim Jong-un.
Matamshi haya ya Korea Kaskazini yanakuja siku chache tu tangu rais Trump asema kuwa kuna uwezekano mkutano wake na Kim Jong-un usifanyika katika tarehe iliyopangwa nchini Singapore.