Pata taarifa kuu

Mwaka mmoja Baadaye, wanawake na wasichana wanabeba mzigo wa mgogoro wa Sudan

Msikilizaji jumatatu ya wiki ijayo, Aprili 15 itakuwa ni mwaka mmoja kamili tangu kuanza kwa vita nchini Sudan, mzozo ambao umesababisha mamilioni ya raia kukosa makazi na maelfu kuuawa.

Біженки з Судану плачуть, дізнавшись про загибель родичів
Picha ikionesha wanawake wakimbizi kutoka Sudan wakilia baada ya kufahamishwa kuhusu vifo vya jamaa zao. © El Tayeb Siddig / Reuters
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Alhamisi ya tarehe 11 Aprili, shirika linalojihusisha na misaada ya kibinadamu, CARE international, limesema wanawake na wasichana ndio waathiriwa wakubwa, ambapo wamekuwa wakibakwa na hata kukosa huduma za afya, suala ambalo linasema ni kama vita dhidi ya wanawake.

Katika taarifa iliyopewa jina “Kwasababu ni wanawake: Namna mzozo wa Sudan ulivyosababisha vita kwa wanawake na Watoto”, iliangazia kwa kina madhila wanayokabiliwa nayo.

Aidha taarifa hiyo imeongeza kuwa, Mzozo huu umekuwa na matokeo ya kutisha kwa mamilioni, umeharibu kila nyanja ya kijamii ya Sudan, na athari zake zimeenea hadi katika nchi jirani ambazo tayari zinakabiliwa na changamoto zao za ndani za kibinadamu.

Wanaoathirika zaidi ni wanawake na wasichana, kwa kiasi kikubwa kutokana na uhasama, huku wimbi la unyanyasaji wa kijinsia likienea, maisha ya watu yakiharibiwa, miundombinu, pamoja na huduma za afya na sasa uhaba wa chakula na njaa inayotarajiwa.

 

Tunashuhudia vita dhidi ya wanawake na wasichana, huku kukiwa na ongezeko la vitendo vya ukatili nchi nzima," alisema Abdirahman Ali, Mkurugenzi CARE nchini Sudan.

 

"Hata kabla ya mzozo huu, wanawake na wasichana milioni 3 walikuwa wakiishi kwa hofu ya unyanyasaji wa kingono au kijinsia. Idadi hiyo sasa imeongezeka kwa karibu asilimia 60. Takwimu hizi ni za kutisha na zinafichua ukweli wa ukatili wa mzozo huu na mzigo mkubwa uliowekwa kwa wanawake na wasichana wa Sudan, haswa wale wanaolazimika kukimbia makazi yao, huku hali ikizidi kuwa mbaya kila kukicha.” Alisema Abdirahman.

 

Ripoti ya CARE, imetolewa siku chache kabla ya kufanyika kwa mkutano wa Kimataifa wa Kibinadamu huko Paris, Aprili 15, 2024, ambapo shirika hili linahimiza nchi wanachama na wafadhili kushughulikia janga hili la kibinadamu.

Kadhalika linatoa wito wa kuwepo kwa umoja katika kuweka kipaumbele cha usawa wa kijinsia na kushughulikia mahitaji maalum ya wanawake na wasichana nchini Sudan.

Katika hatua nyingine mashirika ya misaada yameendelea kufanya tathmini ya hali ilivyo nchini Sudan na kutumia taarifa hizo kutatua changamoto zinazowakabili wanawake.

 

“Mashirika ambayo yanahusika katika kufikia raia, yanaendelea kutathmini hali ya wasichana na wanawake, na kutumia zile taarifa ambazo wanapata kuweza kuwafikia wale watu ambao wanahitaji msaada n asana sana kutoa kipaumbele kwa wanawake. Anasema Maina Kingori, mkurugenzi wa masuala ya kibinadamu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutoka shirika la CARE.

 

Wanawake na wasichana ni sehemu kubwa ya watu karibu milioni 8 na laki 5 waliokimbia makazi yao kwa lazima, huku karibu wajawazito 150,000 hawawezi kupata huduma za afya, wakati theluthi mbili ya vituo vya afya havifanyi kazi.

 

00:39

Maina Kingori mkurugenzi wa masuala ya kibinadamu kwenye ukanda wa Afrika Mashariki na Kati kutoka shirika la CARE

Wanawake wanaokabiliwa na njaa hujiamulia kufanya zaidi ya uwezo na kujihusisha katika vitendo vya ngono ili waendelee kuishi au ndoa ya kulazimishwa kama inavyofafanuliwa katika muhtasari wa taarifa ya CARE, ambapo kati ya watu milioni 4.86 wanaokabiliwa na njaa nchini Sudan, milioni 1.2 ni wanawake wajawazito, na wanaonyonyesha wanaokabiliwa na utapiamlo.

Licha ya kukabiliwa na changamoto hizi, wanawake nchini Sudan wameonesha ujasiri wa hali ya juu na wakutia moyo, imesema taarifa ya shirika hilo.

Haya yanajiri wakati huu umoja wa Mataifa, ukionya kuwa mzozo wa kibinadamu uliosababishwa na vita ya Sudan, unatarajiwa kuwa mbaya zaidi katika siku za usoni, ambapo mataifa jirani huenda yakakabiliwa na njaa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.