Pata taarifa kuu

Côte d'Ivoire yampokea rais wa Italia kuzungumzia nishati na uhamiaji

Rais wa Italia Sergio Mattarella yuko ziarani nchiniCôte d'Ivoire tangu siku ya Jumatano ambapo amekutana na mwenzake Alassane Ouattara kujadili ushirikiano kati ya nchi hizo mbili katika nyanja ya nishati na masuala ya uhamiaji.

Marais wa Italia na Côte d'Ivoire Sergio Mattarella na Alassane Ouattara mjini Abidjan.
Marais wa Italia na Côte d'Ivoire Sergio Mattarella na Alassane Ouattara mjini Abidjan. © AFP
Matangazo ya kibiashara

"Tuna ushirikiano katika sekta ya nishati na makampuni yetu ya Eni na Petroci ambayo yamegundua amana mbili muhimu (mafuta na gesi), na kuifanya Côte d'Ivoire kuwa mhusika katika uwanja huu," amesema rais wa Italia wakati wa mkutano na waandishi wa habari huko Abidjan.

Kampuni kubwa ya Italia Eni ilianza mwishoni mwa mwezi wa Agosti, kwa kushirikiana na kampuni ya Côte d'Ivoire ya Petroci, uzalishaji wa mafuta na gesi asilia kutoka eneo la "Baleine", uzalishaji ambao unaweza kufikia mapipa 150,000 ya mafuta kwa siku na futi za ujazo milioni 200 ya gesi kwa siku.

Mwezi uliopita, Mkurugenzi Mtendaji wa Eni Claudio Descalzi alitangaza ugunduzi wa amana mpya, inayoitwa "Calao", yenye uwezo wa mapipa ya 1 hadi 1.5 bilioni ya mafuta. Rais Mattarella, ambaye nafasi yake ni ya heshima, atatembelea shughuli za kituo cha kusukuma maji kwenye amana ya "Baleine" siku ya Alhamisi.

Masuala ya uhamiaji haramu pia yamejadiliwa na marais hao wawili wakati wa mkutano wao Jumatano asubuhi. "Nilithibitisha tena utayari wa Côte d'Ivoire kufanya kazi ili kupambana na uhamiaji haramu kuelekea Italia," alisema Bw. Ouattara. Mwanzoni mwa 2023, raia wa Côte d'Ivoire walikuwa taifa la pili kuwakilishwa miongoni mwa raia wa Kusini mwa Jangwa la Sahara waliotua Italia, kulingana na Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Kuhudumia Wakimbizi (UNHCR).

Mwishoni mwa mwezi wa Januari, Italia iliandaa mkutano wa kilele kwa Afrika kuwasilisha mpango wa msaada wa euro bilioni 5.5 kwa bara hilo, ukiungwa mkono na mkuu wa serikali ya mrengo mkali wa kulia Giorgia Meloni, kwa kubadilishana na kuongezeka kwa ushirikiano katika uhamiaji. Kisiwa cha Lampedusa, kilichoko takriban kilomita 145 kutoka pwani ya Tunisia, ni mojawapo ya sehemu kuu za kuwasili kwa wahamiaji wanaovuka bahari ya Mediterania kufika Ulaya.

"Tuna hakika ya ushirikiano ambao lazima uwe wa usawa na kuzingatia kuheshimiana," Bw. Mattarella alisema Jumatano. Marais hao wawili hatimaye walijadili hali katika Sahel, ambapo nchi kama Burkina Faso, Mali na Niger zinakabiliwa na ghasia za mara kwa mara za wanajihadi na zinatawaliwa na tawala za kijeshi zilizoingia madarakani kwa njia ya mapinduzi.

"Tulielezea wasiwasi wetu kuhusu hali ya kisiasa na usalama katika Sahel ambayo inaendelea kuwa mbaya," alisema rais wa Italia. Bw. Mattarella anatarajiwa kuondoka Côte d'Ivoire siku ya Alhamisi kuelekea nchi jirani ya Ghana.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.