Pata taarifa kuu

Aliyekuwa mkuu wa majeshi atekwa nyara nchini Burkina Faso

Mkuu wa zamani wa jeshi nchini Burkina Faso, Luteni Kanali Évrard Somda, alitekwa nyara siku ya Jumapili akiwa nyumbani kwake huko Ouagadougou na "watu wenye silaha", kulingana na shirika la habari la AFP likinukuu vyanzo vya karibu naye siku ya Jumatatu.

Brigedia Jenerali Gilbert Ouédraogo alichukua uongozi wa jeshi la kitaifa Jumanne hii huko Ouagadougou.
Brigedia Jenerali Gilbert Ouédraogo alichukua uongozi wa jeshi la kitaifa Jumanne hii huko Ouagadougou. AFP - OLYMPIA DE MAISMONT
Matangazo ya kibiashara

"Alitekwa nyara jana (Jumapili) akiwa nyumbani kwake na watu waliokuwa na silaha: walizingira eneo alikokuwa akiishi, wakaizingira nyumba yake kabla ya kumkamata," kilisema chanzo cha usalama kilicho karibu na afisa huyo.

"Haijulikani kama alikamatwa kwa amri ya jeshi au mahakama, au kama ni utekaji nyara mwingine," kimesema chanzo kingine kilicho karibu na mkuu wa zamani wa jeshi, kikithibitisha habari hiyo. Chanzo hicho kimeeleza kwamba "hakuonyesha upinzani wowote" na "aliwafuata watu waliokuja kumchukua na kumpeleka kusikojulikana".

Akiwa ameachishwa kazi mwezi Oktoba baada ya kukamatwa kwa maafisa wanne, wakiwemo wawili waliokuwa washirika wake wa karibu walioshukiwa kuhusika katika "njama ya kuhatarisha usalama wa taifa", kitendo ambacho utawala wa kijeshi ulioko madarakani ulidai kuzima, Luteni Kanali Evrard Somda hakuwa anaondoka nyumbani kwake, kulingana na dugu zake.

Katikati ya mwezi wa Desemba, alihojiwa na mahakama ya kijeshi kama shahidi, kama sehemu ya uchunguzi uliofunguliwa katika madai ya "njama ya kuhatarisha usalama wa taifa", kitendo kinachohusisha makamanda wawili wa vitengo maalum vya jeshi, kulingana na vyanzo vya mahakama.

Rafiki yake mwengine wa karibu, mfanyabiashara mashuhuri, Sansan Anselme Kambou, alitekwa nyara katikati ya mwezi wa Septemba na maafisa wa kijasusi wa Burkina Faso. Mwanzoni mwa mezi wa Novemba, mahakama ya Ouagadougou iliamuru kuachiliwa kwake, uamuzi ambao bado haujatekelezwa, kulingana na familia yake.

Visa kadhaa vya utekaji nyara viliripotiwa katika miezi ya hivi karibuni na vyanzo vya ndani huko Ouagadougou. Mwishoni mwa mwezi wa Desemba, Ablassé Ouédraogo, Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje wa Burkina Faso na naibu mkurugenzi mkuu wa Shirika la Biashara Duniani (WTO), walitekwa nyara na "watu" waliodai kuwa wa "maafisa wa polisi wa taifa", kulingana na chama chake cha kisiasa, Le Faso Autrement.

Burkina Faso, inayoongozwa na wanajeshi baada ya kufanya mapinduzi mawili ya mwaka 2022, inabiliwa tangu mwaka 2015 na ghasia za wanajihadi zinazotokana na vuguvugu la wapiganaji wenye mfungamano na Al-Qaeda na kundi la Islamic State. Vurugu hizi zimesababisha vifo vya takriban watu 20,000 na zaidi ya milioni mbili kuwa wakimbizi wa ndani.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.