Liberia: Matokeo ya awali ya urais yanaonyesha Weah na Boakai wanakaribiana
Nairobi – Rais wa Liberia George Weah na mgombea wa upinzani Joseph Boakai wameripotiwa kuachana na nafasi ndogo zaidi katika matokeo ya awali ya uchaguzi wa urais, huku karibu robo tatu ya kura ikiwa imepokelewa na tume ya uchaguzi.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Kwa mujibu wa matokeo ya awali yaliotangazwa na tume ya uchaguzi kwenye taifa hilo hapo jana Jumapili, Weah anaongoza kwa asilimia 43.8 dhidi ya asilimia 43.5 ya Boakai, akiwa na takriban asilimia 73 ya kura.
Kufikia Jumapili, tume hiyo ilikuwa imetangaza matokeo kutoka vituo 4,295 kati ya 5,890 vya kupigia kura nchini humo.
Haya yanajiri wakati huu ECOWAS, ikiwaonya waliokuwa wagombea wa urais nchini Liberia dhidi ya kuanza kujitangaza washindi wakati huu tume ya uchaguzi ikiendelea na hesabu ya kura, ECOWAS ikisema hilo litachangia vurugu.
Pia imezitaka pande zote kudumisha amani wakati wakisubiri matokeo, na kuongeza kuwa watawajibishwa kwa vitendo vyovyote vinavyoweza kusababisha vurugu na uvunjifu wa amani. Rais Weah anawania muhula wa pili madarakani.
Boakai, ambaye aliibuka wa pili katika uchaguzi uliopita, alikuwa naibu wa Ellen Johnson Sirleaf alipokuwa rais.
Mshindi lazima apate angalau asilimia 50 ya kura ili kuepuka duru ya pili ya uchaguzi.
Raia wa Liberia walipiga kura tarehe 10 Oktoba kumchagua rais, wajumbe wa baraza la wawakilishi na sehemu ya wabunge wa Seneti.