Madagascar: Viongozi wa upinzani wazuiliwa kufanya mkutano
Nairobi – Maofisa wa usalama nchini Madagascar wamewafyatulia mabomu ya kutoa machozi viongozi wa upinzani waliokuwa wanaoongoza maandamano jijini Antananarivo, hatua inayokuja wakati huu joto la kisiasa likiendelea kupanda kuelekea uchaguzi wa urais wa mwezi ujao.
Imechapishwa:
Wagombea wa urais kumi na mmoja kati ya 13 wanaowania kiti cha urais, walikuwa wametoa wito kwa wafuasi wao kuandamana dhidi ya kile wanachodai ni kupendelewa kwa rais wa sasa Andry Rajoelina.
Waandamanaji hao wamesambaratishwa na maofisa wa polisi kabla ya kuwasili katika eneo walikokuwa wamekusudia kukutana.
Rais wa zamani Marc Ravalomanana ambaye pia ni mojawapo wa wanasiasa wa upinzani wanaowania katika uchaguzi huo, alikuwa miongoni mwa waandamanaji.
Waandaaji wa mkutano huo hawakuwa wamepata kibali cha kufanya hivyo kutoka kwa vyombo vya usalama.
Wapiga kura nchini Madagascar, mojawapo ya mataifa maskini duniani licha ya utajiri wa rasilimali asili, wanapiga kura kumachagua rais wao mpya tarehe 9 ya mwezi Novemba.
Rajoelina mwenye umri wa miaka 49, alijiuzulu kutoka mwezi uliopita kwa mujibu katiba ya nchi hiyo akitaka kuwania tena katika uchaguzi wa mwaka huu.