Pata taarifa kuu

Sudan Kusini:Uchaguzi utafanyika Desemba mwaka 2024

Serikali nchini Sudan Kusini, imetangaza  na kuthibitisha kuwa uchaguzi mkuu wa kwanza ambao umekuwa ukisubiriwa kwa muda mrefu tangu nchi hiyo ilipoanza kujitawala mwaka 2011 , sasa utafanyika mwezi Desemba mwaka  2024.

Uchaguzi wa Sudan utafanyika Desemba mwaka  2024
Uchaguzi wa Sudan utafanyika Desemba mwaka 2024 © @Reuters
Matangazo ya kibiashara

Mwezi wa saba mwaka huu Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir aliahidi kuwa uchaguzi uliocheleweshwa  na ambao unatarajiwa kufanywa mwaka ujao utaendelea kama ilivyopangwa na kuwa atagombea kiti cha urais.

Hapo jana Waziri wa Habari Michael Makwei, alisema kuwa uchaguzi huo utafanyika bila ya kuwepo na Katiba mpya.

Aidha, alisema kuwa  ni sharti uchaguzi huo ufanyike ili kuwapata wawakilishi waliochaguliwa na wananchi, wakiwemo wabunge.

Tunaweza kufanya uchaguzi tukiwa na katika tuliyo nayo sasa. Bunge la sasa haliwezi kuidhinisha katika mpya. Bunge hili haliwakilishi matakwa ya wananchi wa Sudan.

Hata hivyo, chama kikuu cha upinzani cha SPLM-IO, kinachoongozwa na Makamu wa Kwanza wa rais Riek Machar, kinaishtumu serikali kuharakisha mchakato wa uchaguzi kabla ya utekelezwaji wa mkataba wa amani wa mwaka 2018, kama anavyoeleza Puok Both Baluang, msemaji wa chama hicho.

 

 Tunahitaji kukamilishwa kwa vipengele vyote vya mkataba wa amani na hasa katiba ambayo imetajwa kwenye mapatano ya amani. Tunahitaji katiba ya kudumu.

Upinzani umekuwa ukimshtumu rais Kiir kwa kutokuwa na utashi wa kisiasa kuhakikisha kuwa uchaguzi huo unafanyika, huku Umoja wa Mataifa kupitia mjumbe wake nchini humo Nicholas Haysom akionya kuwa viongozi wa serikali na upinzani wanapaswa kutekeleza mkataba wa amani, na kuandaa uchaguzi huo kama ilivyopangwa.

 

Ghasia miongoni mwa jamii za Sudan Kusini zinaendelea kuongezeka pamoja na shinikizo la kuongezeka kwa ufinyu wa rasilimali huku maelfu ya watu wakiendelea kuingia nchini humo wakikimbia mapigano katika nchi jirani ya Sudan.  

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.