Pata taarifa kuu

Niger, Mali: Umoja wa Mataifa waonya kuhusu uhaba wa chakula katika Sahel

Umoja wa Mataifa umetoa tahadhari kuhusu uhaba wa chakula nchini Niger, ambako zaidi ya watu milioni 3 ni waathirika, na nchini Mali, ambako watoto 200,000 wana hatari ya kufa kwa njaa kama hakutapatikana msaada wowote wa kibinadamu.

Mwanamke akitayarisha chakula huko Niamey, Niger, Julai 29, 2023.
Mwanamke akitayarisha chakula huko Niamey, Niger, Julai 29, 2023. © AP
Matangazo ya kibiashara

Nchini Niger, ambako jeshi lilichukua mamlaka mwishoni mwa mwezi Julai, zaidi ya watu milioni 3.3, sawa na asilimia 13 ya raia wote, wako katika hali ya uhaba mkubwa wa chakula, mashirika ya Umoja wa Mataifa yamesema katika taarifa yao ya pamoja.

Kwa vile bei za vyakula zimeongezeka hadi 21% katika mwezi uliopita, hali hii inaweza kuwa mbaya zaidi, Umoja wa Mataifa unaonya.

"Zaidi ya watu milioni 7 (karibu 28% ya raia) wanaweza kuangukia katika uhaba mkubwa wa chakula kutokana na kupanda kwa bei na kukosekana kwa mapato, hali inayosababishwa na mzozo wa sasa wa kisiasa," unaonya Umoja wa Mataifa, ambao una wasiwasi kuhusu vikwazo vya upatikanaji wa misaada ya kibinadamu.

Zaidi ya tani 7,300 za chakula kutoka Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) zimekwama kutokana na kufungwa kwa mipaka. Na mpango wa kibinadamu wa Umoja wa Mataifa kwa Niger kwa mwaka 2023, unaokadiriwa kuwa dola milioni 584, unafadhiliwa kwa asilimia 40 pekee.

Umoja wa Mataifa "una wasiwasi mkubwa kuhusu kusimamishwa au kukatizwa kwa ufadhili kutoka kwa wafadhili" kutokana na mapinduzi ya kijeshi yaliyompindua Rais Mohamed Bazoum mnamo Julai 26.

Kulingana na shirika la Umoja wa Mataifa, karibu robo ya wakazi wa Mali wanakabiliwa na uhaba wa chakula wa wastani au mkubwa, na "kwa mara ya kwanza nchini humo, zaidi ya watu 2,500 wanatishiwa na njaa katika eneo la Ménaka, wengi wao wakiwa watoto" .

Kilio hiki cha hofu kinakuja wakati tume ya Umoja wa Mataifa ya kulinda amani nchini Mali (MINUSMA) imeanza kuondoka nchini humo na Umoja wa Mataifa una wasiwasi kuhusu athari za uondoaji huu unaotakiwa na Bamako katika operesheni za kibinadamu zilizolindwa hapo awali na walinda amani.

"Mali inapitia mzozo mgumu wa kibinadamu na inahitaji usaidizi wa haraka ili kuepusha janga kwa watoto, ambao kwa mara nyingine tena wanalipa gharama ya mgogoro ambao hawahusiki," ame shutumu Ted Chaiban, afisa wa operesheni za kibinadamu kutoka UNICEF.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.