Pata taarifa kuu

Chakwera: Tukubali tuko nyuma kwa maendeleo ya teknolojia

Imani za kishirikina, upotoshaji ni miongoni mwa mambo yaliyotajwa kuwa yanakwamisha ukuaji wa maendeleo ya teknolojia barani Afrika, na kwamba ni lazima tamaduni Fulani ziachwe ili kufikia lengo.

Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, akihutubia wakati wa mkutano wa Transform Afrika uliofanyika nchini Zimbabwe. 26/04/2023
Rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, akihutubia wakati wa mkutano wa Transform Afrika uliofanyika nchini Zimbabwe. 26/04/2023 © State House Malawi
Matangazo ya kibiashara

Ni kauli ya rais wa Malawi, Lazarus Chakwera, akiwanyooshea kidole watu wanaoshikilia Imani potofu kuhusu ukuaji wa teknolojia barani Afrika, akisema wakati umefika kwa bara hilo kukumbatia mabadiliko ya kuteknolojia.

“Matokeo ya ucheleweshaji huu ni kwamba Afrika imeachwa nyuma, tumeachwa nyuma katika sekta ya kilimo na sekta nyingine nyingi. Na ukweli ni kwamba naweza kuwaambia kuwa Afrika imeachwa nyuma sana na huenda tusiwafikie wengine ikiwa tutaendelea kutumia njia zilezile za wenzetu ambao kwa sasa wametuacha mbali sana kwa miaka kimaendeleo.”

Aidha kwa upande wake rais wa Rwanda ambaye pia ni mwenyekiti wa bodi wa taasisi ya Smart Afrika, anasema mabadiliko na maendeleo ya teknolojia hayaepukiki ikiwa nchi zao zinataka kupiga hatua.

“Tunahitaji kuwa na utambuzi wa kirahisi wa kidijiti wa watu na biashara katika maeneo yote ya mipaka, huku tukitumia teknolojia kupunguza vikwazo kwa biashara. Mambo yote haya yako ndani ya uwezo wetu kuyafanikisha.”
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, wakati akihutubia mkutano wa Transform Afrika, uliofanyika nchini Zimbabwe. 26/04/2023.
Rais wa Rwanda, Paul Kagame, wakati akihutubia mkutano wa Transform Afrika, uliofanyika nchini Zimbabwe. 26/04/2023. © Rwanda Presidency
Kwa upande wake mwenyeji wa mkutano huu wa 6 wa Transform Afrika, rais wa Zimbabwe, Emmerson Munangagwa, amesema ni lazima nchi za Afrika zitumie vizuri rasilimali ilizonazo kwa kutumia teknolojia ili kurahisisha na kuharakisha maendeleo.

“Ushirikiano ni muhimu kwa bara la Afrika kusonga mbele na kujenga uwezo wa sayansi na teknolojia. Hivyohivyo ni lazima tuhuishe suala la sayansi na teknolojia  kwa kuwa na ubunifu na mikakati ya malengo ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii ya bara la Afrika.”

Kwa wadau wengi wa maendeleo barani Afrika ni suala la muda tu kabla Afrika haijapiga hatua katika kutumia ipasavyo teknolojia kubadili sekta ya kilimo, afya na elimu, wakati huu ambapo tayari nchi nyingi zinaenda na wakati.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.