Pata taarifa kuu

Baraza la Usalama kuzuru DRC, iliyokumbwa na ghasia Mashariki

Ujumbe kutoka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa unaanza ziara ya siku tatu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo siku ya Alhamisi, ambapo mapigano yanaendelea kurindima mashariki mwa nchi hiyo kati ya jeshi na waasi wa M23, duru za Umoja wa Mataifa zimesema.

Wanajeshi wa Kongo katika mji wa Bunagana.
Wanajeshi wa Kongo katika mji wa Bunagana. AFP - HABIBOU BANGRE
Matangazo ya kibiashara

Baada ya matangazo kadhaa ya kusitisha mapigano kutotekelezwa katika miezi ya hivi karibuni, usitishaji mapigano ulipaswa kuanza kutekelezwa Jumanne. Siku moja kabla, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres aliwataka waasi hao kutii mapatano hayo, wakati mwishoni mwa juma lililopita Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron, aliyezuru Kinshasa, alitishia pande zinazozozana kuziwekea vikwazo.

Lakini mapigano yanaendelea kurindima katika mkoa wa Kivu Kaskazini, ambako M23, waasi ambao walichukua silaha mwishoni mwa 2021, wameendelea tangu siku ya Jumanne kupanua eneo lao. Kinshasa inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono waasi hao, madai ambayo yalithibitishwa na wataalamu wa Umoja wa Mataifa na kulaaniwa na nchi kadhaa za Magharibi, ingawa Kigali inakanusha.

"Tunazihimiza pande zote kusitisha mapigano na wale wote ambao hawana shughuli yoyote nchini DRC kurejea nyumbani," Nicolas de Rivière, balozi wa Ufaransa katika Umoja wa Mataifa, aliwaambia waandishi wa habari mjini New York siku ya Jumatano kabla ya kuondoka kuelekea Kinshasa.

Ujumbe wa Baraza la Usalama, unaotarajiwa Alhamisi jioni katika mji mkuu wa DRC, ambako utakutana na mamlaka, ikiwa ni pamoja na Rais Félix Tshisekedi, siku ya Jumamosi na Jumapili, utafanya ziara mjini Goma , mji mkuu wa Kivu Kaskazini, mji wa zaidi ya watu milioni 1, unaopakana na Rwanda upande wa mashariki, Ziwa Kivu upande wa kusini na waasi wa M23 upande wa kaskazini na magharibi.

Wawakilishi wa Baraza wanakusudia "kutathmini hali ya usalama na kibinadamu katika mkoa wa Kivu Kaskazini", Ujumbe wa Umoja wa Mataifa nchini humo (MONUSCO) umebaini katika taarifa.

Mwaka uliopita, zaidi ya watu 800,000 waliathiriwa na mapigano kati ya jeshi na waasi wa M23, Farhan Haq, naibu msemaji wa Antonio Guterres, alisema siku ya Jumatano.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.