Pata taarifa kuu
KIFO - CHRISTIAN ATSU

Mwili wa Christian Atsu wapatikana baada ya tetemeko la ardhi, Uturuki

Mashabiki wa mchezo wa soka barani Afrika na kwingineko duniani, wanaomboleza kifo cha mchezaji wa timu ya taifa ya Ghana Christian Atsu wiki mbili baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi nchini Uturuki, alikokuwa anacheza soka.

Christian Atsu, mshambuliaji wa Ghana.
Christian Atsu, mshambuliaji wa Ghana. © AFP - PAUL ELLIS
Matangazo ya kibiashara

Atsu alitoweka tangu Februari 6 baada ya kutokea kwa tetemeko la ardhi nchini Uturuki, alikokuwa anacheza soka katika klabu ya Hatayspor.

Baada ya kumtafuta siku kadhaa, wakala wa mchezaji huyo ambaye amewahi kucheza soka katika klabu ya Everton, Chelsea na Newcastle siku ya Jumamosi, amethibitisha kupatikana kwa mwili wa Atsu katika vifusi vya jengo alilokuwa anaishi katika êneo la Antakya, Hatay.

Wizara ya mambo ya nje ya Ghana kwenye taarifa yake, imesema imesikitishwa na taarifa za kifo cha Atsu.

Kaka mkubwa na pacha wake Christian Atsu na afisa wa ubalozi wa (Ghana) walikuwepo kwenye eneo hilo wakati mwili ulipopatikana. Imesema taarifa ya wizara hiyo.

Kifo cha Atsu pia kimethibitishwa na Shirikisho la soka nchini Ghana, ambalo limesema mwili wa mchezaji huyo ulipatikana leo asubuhi, na kusema tangu kutoweka kwake, kimekuwa ni kipindi kigumu, na kumkumbuka kama mchezaji mahiri wakati wa uhai wake.

Atsu alijiunga na klabu ya Hatayspor Septemba 2022, akitokea klabu ya Al-Raed nchini Saudi Arabia.

Itakumbukwa kwamba mwaka 2015, katika kuwania kombe la Mataifa ya Afrika, Atsu alifunga mabao matatu 3-0 dhidi ya Guinea katika robo-fainali na ni katika michuano hiyo ambapo alitwaa tuzo za mchezaji bora.

Mbali na kuichezea timu ya taifa ya Ghana mara 65, pia alikuwa sehemu ya kikosi cha Ghana kwenye Kombe la Dunia la 2014 nchini Brazil.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.