Pata taarifa kuu

Ishirini wauawa katika makabiliano kati ya waandamanaji na vikosi vya usalama Somaliland

Takriban watu 20 wameuawa katika eneo lililojitenga la Somalia la Somaliland katika makabiliano kati ya waandamanaji wanaoipinga serikali na vikosi vya usalama kwa siku kadhaa, kulingana na daktari mmoja katika hospitali ya serikali.

Vikosi vya jeshi vya Puntland na Somaliland vilipambana vikali msituni karibu na mpaka wao, kilomita 30 kusini mwa eneo la Dhahar, Julai 18, 2016.
Vikosi vya jeshi vya Puntland na Somaliland vilipambana vikali msituni karibu na mpaka wao, kilomita 30 kusini mwa eneo la Dhahar, Julai 18, 2016. GOOGLE MAPS
Matangazo ya kibiashara

Kwa zaidi ya wiki moja, maafisa wa polisi na wanajeshi wamekuwa wakipambana na waandamanaji huko Laascaanood, mji ulioko mashariki mwa Somaliland ambao unazozaniwa kati ya Somaliland na jirani yake Puntland, moja ya majimbo ya Somalia yanayojitawala.

Waandamanaji hao wanaitaka Somaliland kukabidhi udhibiti wa mji huo kwa Puntland. Pia wanashutumu vikosi vya usalama kwa kushindwa kukomesha hali ya ukosefu wa usalama katika jiji hilo.

"Somaliland inaikalia Laascaanood kwa nguvu na imeshindwa kuilinda. Tunawataka [wakazi wa Somaliland] kuondoka," Adaan Jaamac Oogle, msemaji wa waandamanaji, ameliambia shirika la habari la Reuters.

"Hatuwezi kuvumilia umwagaji damu wa raia unaoendelea," ameongeza.

Mohamed Farah, daktari katika hospitali ya umma ya Laascaanood, ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba takriban watu 20 waliuawa na makumi ya wengine kujeruhiwa.

Msemaji wa polisi hakujibu mara moja simu kutoka kwa shirika la habari la Reuters lililopomuomba ajibu kuhusiana na madai hayo.

Makamu wa Rais wa Puntland Ahmed Elmi Osman Karash anashutumu vikosi vya usalama kwa vurugu.

"Jeshi la Somaliland linachofanya ni mauaji ya raia," ameliambia shirika la habari la Reuters kwa njia ya simu.

Mahad Ambaashe Elmi, kamanda mkuu wa jeshi la Somaliland, hakujibu simu ya shirika la habari la Reuters.

Siku ya Jumamosi katika taarifa yake, Waziri wa Habari wa Somaliland Salebaan Ali Koore aliwataka waandamanaji kusitisha maandamano yao na kuanza mazungumzo na serikali.

Somaliland ilijitenga na Somalia mwaka 1991 lakini haikutambuliwa kimataifa kwa uhuru wake. Eneo hilo limekuwa na amani zaidi, huku Somalia ikikabiliwa na miongo mitatu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.