Pata taarifa kuu
USALAMA-JAMII

Nigeria: Watu wenye silaha wawateka nyara watoto 39 shambani

Kundi la wahalifu limewateka nyara watoto 39 wanaofanya kazi katika shamba moja kaskazini-magharibi mwa Nigeria kwa ajili ya fidia, polisi na afisa wa eneo hilo wamesema siku ya Jumatano.

Vikosi vya usalama nchini Nigeria vinawashikilia wanaume watatu waliotambuliwa kama watekaji nyara wa wanafunzi Septemba 23, 2021 huko Abuja.
Vikosi vya usalama nchini Nigeria vinawashikilia wanaume watatu waliotambuliwa kama watekaji nyara wa wanafunzi Septemba 23, 2021 huko Abuja. AP - Gbemiga Olamikan
Matangazo ya kibiashara

Siku ya Jumapili, makumi ya watu wenye silaha wakiwa kwenye pikipiki walivamia shamba nje ya kijiji cha Mairuwa katika jimbo la Katsina, na kuwateka nyara watoto hao 39, vyanzo vimesema. Magenge yenye silaha, yanayojulikana nchini humo kama "majambazi", yanatishia majimbo ya kaskazini-magharibi na kati ya nchi hii ya Nigeria yenye watu wengi zaidi barani Afrika, kupora, kuteka nyara na kuua wanakijiji.

Kwa kawaida mateka hao huachiliwa baada ya kulipa fidia kwa magenge yanayopata hifadhi katika msitu mkubwa wa Rugu, unaozunguka majimbo ya Zamfara, Niger, Katsina na Kaduna. "Majambazi walivamia shamba la Mairuwa na kuwachukua wafanyakazi vijana," msemaji wa polisi wa jimbo la Katsina Gambo Isah amesema.

"Maafisa wetu wametumwa katika eneo hilo kwa dhamira ya kuwaokoa mateka na kuwatia nguvuni wahalifu," ameongeza Bw. Isah, bila kutoa maelezo zaidi. Afisa wa eneo hilo katika wilaya ya Faskari, ambako kijiji cha Mairuwa kinapatikana, amesema kulikuwa na wafanyakazi kadhaa wakifanya kazi katika shamba moja.

"Wafanyakazi watu wazima, ambao waliweza kukimbia kwa kasi zaidi, walifanikiwa kutoroka lakini watoto 39, ambao hawakuweza kuwashinda mbio majambazi, walikamatwa," chanzo kimoja kimesema kwa sharti la kutotajwa.

Hapo awali, meneja wa shamba hilo alikuwa amefikia makubaliano na majambazi: pesa kwa ahadi ya mavuno kuweza kufanyika. Lakini watu wenye silaha walipokea malipo ya chini tu, afisa wa wilaya ya Faskari amesema.

"Ni dhahiri kwamba majambazi walikuwa na hasira kwamba shughuli ilikuwa imeanza tena shambani bila pesa kamili kulipwa," ameongeza.

Wilaya ya Faskari, iliyoko mpakani na jimbo la Zamfara, inaishi chini ya vitisho vya mara kwa mara vya kutekwa nyara na majambazi hao, kulingana na chanzo hiki.

Rais Muhammadu Buhari anakosolewa vikali na wakosoaji baada ya mihula miwili inayoashiria hasa kuongezeka kwa ukosefu wa usalama, miezi minne kabla ya uchaguzi wa rais ambapo hatawania tena kwenye kiti cha urais, kwa mujibu wa Katiba.

Kando na majambazi, Nigeria, ambayo ina wakazi karibu milioni 215, pia inakabiliwa na makundi ya kijihadi kaskazini mashariki na machafuko ya kujitenga kusini mashariki.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.