Madrid yathibitisha vifo vya Wahispania wawili nchini Burkina Faso
Wanahabari wawili kutoka Uhispania waliuawa baada ya kulengwa na shambulio la kushtukiza lililotekelezwa na kundi la watu wenye silaha mashariki mwa Burkina Faso dhidi ya doria inayopambana na ujangili Jumatatu wiki hii, Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez amesema.
Imechapishwa:
Raia wa Ireland pia aliuawa katika shambulio hilo, kulingana na vyanzo vitatu vya usalama nchini Burkinabe ambavyo havikutaka majina yao yatajwe. Kulingana na moja ya vyanzo hivi, mwanajeshi wa Burkina Faso pia hajulikani aliko kufuatia shambulio hili.
Serikali ya Burkina Faso imethibitisha kuwa watu wanne - ikiwa ni pamoja na raia watatu wa kigeni - walitoweka baada ya shambulio hili lakini imebainisha kuwa waathiriwa hao hawakutambuliwa rasmi kwenye picha za maiti zao zilizorushwa kwenye mitandao ya kijamii.
Waziri Mkuu wa Uhispania hata hivyo amethibitisha kwenye mtandao wa Twitter vifo vya waandishi hao wawili. "Habari mbaya kabisa imethibitishwa," ameandika Pedro Sanchez.
Se confirma la peor de las noticias. Todo el cariño para los familiares y allegados de David Beriain y Roberto Fraile, asesinados en Burkina Faso. Y nuestro reconocimiento a quienes, como ellos, realizan a diario un periodismo valiente y esencial desde las zonas de conflicto.
— Pedro Sánchez (@sanchezcastejon) April 27, 2021
Ireland yashirikiana na washirika wa kimataifa kuwatambua wahusika
Wizara ya Mambo ya nje ya Ireland ilisema Jumatatu jioni kwamba ilipewa taarifa hiyo mbaya na kusisitiza kuwa inafanya kazi na "washirika wa kimataifa juu ya hali hiyo".
Kundi hilo liliripotiwa kutoweka baada ya washambuliaji wenye silaha kushambulia msafara wa vikosi vya usalama na raia wa kigeni Jumatatu asubuhi kwenye barabara inayoelekea kwenye hifadhi kubwa ya msitu wa Pama mashariki mwa nchi, serikali ya Burkina Faso imesema.