Pata taarifa kuu
MALAWI

Malawi: Upinzani wakataa kutambua matokeo, Mutharika ataka umoja

Chama kikuu cha upinzani nchini Malawi kimeenda mahakamani kupinga matokeo ya uchaguzu mkuu wa urais wa Mei 21, chama hicho kikisema kulikuwa na dosari nyingi wakati wa uchaguzi.

Rais wa Malawi, Peter Mutharika ambaye ameshinda uchaguzi kwa muhula wa pili, picha kutoka maktaba:: 14 November 2013
Rais wa Malawi, Peter Mutharika ambaye ameshinda uchaguzi kwa muhula wa pili, picha kutoka maktaba:: 14 November 2013 AFP/Amos Gumulira
Matangazo ya kibiashara

Lazarus Chakwera, kiongozi wa chama cha Malawi Congress, amesema ni lazima kuwa na uwajibikaji kutokana na baadhi ya watu kukiuka waziwazi sheria za uchaguzi.

"Ni mfumo wa uchaguzi ambao maofisa wa tume wanaweza kutumia wino maalumu katika kufuta matokeo ya kwenye karatasi halisi nchi nzima....na bado watu wasichukuliwe hatua," alisema Chakwera.

Chakwera ambaye aliapata asilimia 35.41 ya kura zote, alishindwa na rais Peter Mutharika ambaye alishinda uchaguzi huo kwa kupata asilimia 38.57 huku wakitenganishwa na kura laki moja na elfu hamsini pekee.

Wakati huu upinzani ukipinga matokeo ya uchaguzi, rais Mutharika baada ya kuapishwa Jumanne ya wiki hii, aliwataka wanasiasa wa upinzani kukubali kushindwa na kuijenga nchi yao.

Mutharika alitumia hotuba yake kuwataka wanasiasa wa upinzani kuungana na kumsaidia kuijenga upya Malawi aliyosema imeendelea kukabiliwa na changamoto za kiuchumi.

"Ni muda wa kusonga. Hakuna muda wa kupigana. Kuna muda wa kuungana, kuungana na kuiendeleza nchi," alisema Mutharika wakati akiwahutubia maelfu ya wafuasi wake kwenye uwanja wa Kamuzu mjini Blantyre.

Rais Mutharika kwa upande wake ametupilia mbali madai ya upinzani, akisema waangalizi wa kimataifa waliutaja uchaguzi wa Mei 21 kama ulikuwa uchaguzi huru na wa haki.

"Ni ushindi kwa utawala wa sheria na demokrasia. Demokrasia imeshinda," alisema rais Mutharika.

Kwa upande wake mgombea mwingine wa upinzani Saulos Chilima ambaye alikuwa makamu wa rais wa Mutharika wakati wa muhula wake wa kwanza, alipata asilimia 20.24 ya kura zote, akiwa amejiondoa kwenye chama tawala kuwania urais.

Yeye kwa upande wake alikubali kushindwa na kumpongeza bosi wake wa zamani kwa ushindi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.