Pata taarifa kuu
ALGERIA-MAANDAMANO-SIASA-UCHAGUZI

Utawala wa Bouteflika waendelea kupoteza uungwaji mkono

Rais wa Algeria anaendelea kupoteza uungwaji mkono kutoka ndani na nje ya chama chake, baada ya Mkuu wa majeshi kuomba Ibara ya 102 ya Katiba ya nchi izingatiwe kwa kuheshimu matakwa ya wananchi.

Maandamano yanayomtaka rais Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu, Algiers Machi 19, 2019.
Maandamano yanayomtaka rais Abdelaziz Bouteflika kujiuzulu, Algiers Machi 19, 2019. © REUTERS/Ramzi Boudina/File Photo
Matangazo ya kibiashara

Jenerali Ahmed Gaid Salah ametaka rais wa nchi hiyo Abdelaziz Bouteflika kutangazwa ameshindwa kuongoza nchi hiyo, hatua inayokuja baada ya majuma kadhaa ya maandamano kupinga kiongozi huyo kuwania urais kwa muhula wa tano.

Katika hotuba yake iliyorushwa kupitia televisheni ya taifa, Jenerali Gaid Salah amesema anaamini madai ya raia yana uhalali na kwamba rais Bouteflika anapaswa kuachia ngazi kupisha uchaguzi mkuu.

Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika akiwa pamoja na Mkuu wa majeshi Ahmed Gaïd Salah, Algiers Juni 27, 2012.
Rais wa Algeria Abdelaziz Bouteflika akiwa pamoja na Mkuu wa majeshi Ahmed Gaïd Salah, Algiers Juni 27, 2012. REUTERS/Ramzi Boudina/File Photo

Wakati huo huo Chama kinachoshirikiana na chama tawala nchini Algeria kuongoza serikali RND, kimeunga mkono kauli ya jeshi, kumtaka rais Abdelaziz Boteflika, kujiuzulu kutokana na kutokuwa na uwezo kuendelea kuongoza kwa sababu za kiafya.

Kiongozi wa chama hicho ambaye ni mshirika wa karibu wa rais Boteflika, amesema kiongozi huyo ameihudumia nchi kwa muda mrefu na ni wakati wa kuondoka.

Maandamano yameendelea kushuhudiwa nchini Algeria licha ya rais Bouteflika, mwenye umri wa miaka 82 kuendelea kusalia madarakani, licha ya kutangaza kuwa hatawania tena urais.

Kwa upande mwengine mwenyekiti wa taasisi ya vijana nchini Algeria, Addad Hakim anasema wao wataendelea na maandamano kwa juma zima kushinikiza kuondoka madarakani kwa wa rais Bouteflika.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.