Ebola yaua zaidi ya watu mia tano nchini DRC
Zaidi ya watu mia tano wamefariki dunia kufuatia mlipuko wa virusi vya Ebola nchini DRCongo huku chanjo ya kupambana na virusi hivyo ikiepusha maelfu ya watu kuathirika kwa maradhi hayo hatari,wizara ya afya nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo imefahamisha.
Imechapishwa:
Kwa mujibu wa waziri wa afya nchini DRC Oly Ilunga Kalenga watu 502 wamefariki dunia huku 271 wakitibiwa baada ya maradhi hayo kuathiri zaidi eneo la mashariki mwa DRC.
Aidha waziri Ilunga ameeleza kuwa mpango wa chanjo ya Ebola umeokoa kiasi cha watu 76,425 na kuzuia idadi kubwa ya vifo.
Waziri Ilunga amesema ana imani kuwa ugonjwa huo umedhibitiwa kusambaa zaidi katika miji mikubwa ya eneo la mashariki.
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo inaendelea kukumbwa na ugonjwa hatari wa Ebola hasa mashariki mwa nchi hiyo, katika mkoa wa Kivu kaskazini.
Mataifa jirani na DRC ikiwemo Uganda, imeendelea kuimarisha upimaji wa afya katika mpaka wake na DRC, kwa hofu ya kusambaa kwa maambukizi ya ugonjwa hatari wa Ebola.