Pata taarifa kuu
COTE D'IVOIRE-USALAM

Wanajeshi waasi waendelea kugoma Cote d'Ivoire

Milio ya risasi ilisikika karibu na ikulu ya rais katika mji mkuu Abidjan, na katika mji wa pili kwa ukubwa wa Bouaké, pamoja na miji mingine muhimu kwa zao la kakao nchini Cote d'Ivoire.

Wanajeshi walioasi wakisalimiana hivi karibuni kwenye mji wa Bouake, Cote d'Ivoire.
Wanajeshi walioasi wakisalimiana hivi karibuni kwenye mji wa Bouake, Cote d'Ivoire. REUTERS/Thierry Gouegnon
Matangazo ya kibiashara

Wanajeshi wanaogoma nchini humo wamefyatua risasi katika miji minne mikubwa nchini Cote d'Ivoie na kukaidi amri ya serikali ya kuwataka waweke chini silaha zao.

Wanajeshi hao waasi, waliomsaidia Alassane Ouattara kuingia madarakani mwaka 2011, wamekuwa wakitofautiana na serikali kuhusu kulipwa malimbikizi yao ya marupurupu.

Shughuli mbalimbali zimezorota nchini Cote d'Ivoire.

Awali Mkuu wa Majeshi nchini humo Sékou Touré alisema idadi kubwa ya wanajeshi hao wanaoasi wanaokadiriwa kuwa 8,000 wamekubali kuweka silaha chini na kurejea kambini baada ya wito wa rais Outtara.

Hata hivyo Jenerali Sékou Touré ameapa kumaliza maasi hayo, ambayo yalitokana na mzozo kuhusu malipo.

“Lakini operesheni ya kijeshi imeanzishwa kwa sababu baadhi ya wanajeshi wameendelea kupuuza maagizo ya wakuu wao, “ Sékou Touré amesema.

Wanajeshi hao waasi wameapa kujibu mashambulio iwapo watakabiliwa na wanajeshi watiifu kwa serikali.

Serikali imepungukiwa na pesa kutokana na kushuka kwa bei ya zao la kakao, jambo linaloifanya vigumu kwa serikali kutimiza madai ya wanajeshi hao.

Mzozo huo wa sasa umezua wasiwasi wa kuzuka tena kwa ghasia zilizoshuhudiwa wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka kumi nchini Ivory Coast, ambavyo vilimalizika mwaka 2011.

Wengi wa wanajeshi hao waasi, ambao walianza kuasi Januari, ni waasi wa zamani ambao walijiunga na jeshi baada ya kumalizika kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.