Pata taarifa kuu
DRC

Maswali yaendelea kusalia kuhusu makubaliano yaliyofikiwa DRC

Licha ya kutiwa saini kwa makubaliano ya kisiasa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, DRC, mwishoni mwa juma, maswali yameendelea kuwa mengi kuliko majibu ya kile kilichokubaliwa na wanasiasa chini ya upatanishi wa maaskofu wa kanisa katoliki nchini humo.

Askofu Fridolin Ambongo, kutoka baraza la maaskofu wa kanisa katoli (Cenco), akitia saini makubaliano ya kisiasa mwishoni mwa juma.rs  1 January 2017, Kinshasa.
Askofu Fridolin Ambongo, kutoka baraza la maaskofu wa kanisa katoli (Cenco), akitia saini makubaliano ya kisiasa mwishoni mwa juma.rs 1 January 2017, Kinshasa. REUTERS/Kenny Katombe
Matangazo ya kibiashara

Mwishoni mwa juma, ujumbe wa maaskofu wa kanisa katoliki walifanikiwa kuzishawishi pande zinazokinzana nchini DRC, kufikia makubaliano na kutia saini mkataba utakaoshuhudia kumalizika kwa mvutano wa kisiasa kuhusu muhula wa rais Joseph Kabila.

Chini ya makubaliano haya, ambapo rais Kabila kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo alitakiwa kuondoka madarakani Desemba 20 mwaka huu, sasa atasalia madarakani hadi pale uchaguzi mwingine utakapofanyika mwishoni mwa mwaka huu.

Katika kipindi cha miezi 12, kile kinachoitwa baraza la mpito litaundwa, na litaongozwa na kiongozi wa upinzani Etienne Tshisekedi na waziri mkuu atateuliwa kutoka upande wa upinzani.

Mkuu wa baraza la maaskofu wa kanisa katoliki nchini DRC, Marcel Utembi, amesema makubaliano haya ni muhimu na yanatoa taswira chanya ya utangamano wa kisiasa nchini humo.

Waangalizi wa kimataifa wamepongeza kufikiwa kwa makubaliano haya, ingawa wameonya kuhusu kazi kubwa iliyoko mbele.

Mkuu wa sera za mambo ya kigeni wa umoja wa Ulaya, Federica Mogherini, katika taarifa yake kwa vyombo vya habari, amesema makubaliano haya lazima yawe ya wazi kuelekea kufikia maridhiano ya kitaifa.

Hata hivyo maswali kadhaa muhimu yameendelea kusalia, moja, ni lini makubaliano haya yataanza kutekelezwa? mbili, Utaratibu utakaotumika kuwapata viongozi utasimamiwaje licha ya kuanishwa kwenye makubaliano? swali la tatu, ni kwanini ujumbe wa muungano wa vyama vinavyomuunga mkono rais Kabila havikutia saini?

Uhalali wa makubaliano haya uko wapi ikiwa tayari kuna makubaliano mengine yaliyohusisha wanasiasa wa upinzani na mashirika ya kiraia ambayo nayo yalitiwa saini na hata kumruhusu rais kabila kukaa madarakani hadi mwaka 2018 na tayari ameshateua waziri mkuu mpya?

Haya ni baadhi ya maswali mtambuka ambayo wataalamu wa siasa za kimataifa na wapatanishi wa kimataifa wanahoji, lakini hata hivyo ikiwa yatatiliwa maanani, basi itashuhudiwa kumalizika kwa mvutano wa kisiasa.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.