Riek Machar apatishiwa matibabu Khartoum
Riek Machar, makamu wa rais wa Sudan Kusini aliyefutwa kwenye wadhifa huo hivi karibuni, yuko katika mji wa Khartoum, ambapo anapatishiwa matibabu, serikali ya Sudan imesema.
Imechapishwa:
Machar yuko katika mji mkuu wa Sudan kwa ajili ya "matibabu", kulingana na taarifa iliyotolewa na serikali ya Sudan Sudan na kuchapishwa na shirika la habari la Sudan la SUNA.
"Sudan hivi karibuni ilimpokea Dk Riek Machar, kwa sababu za kiutu," serikali ya Sudan imesema.
Kwa mujibu wa serikali ya Sudan, aliyekuwa Makamu wa rais wa Sudan Kusini anahitaji "huduma za dharura za matibabu".
"Hali ya afya ya Dk Machar sasa imeimarika. Atakuwa chini ya uangalizi wa matibabu mpaka atakapoondoka kwenda katika nchi ambayo ni chaguo lake," imeongeza taarifa ya serikali.
Baada ya kufutwa kwenye wadhifa wa Makamu wa rais mwezi Julai, Riek Machar alitangazwa kukimbilia katika "nchi salama" ya ukanda wa Afrika ya Mashariki wiki iliyopita na msemaji wake, James Gatdet Diak.