Pata taarifa kuu
BURUNDI

Cnared: Tumeridhishwa na mazungumzo kati yetu na Mkapa

Muungano wa vyama vya upinzani nchini Burundi, Cnared, unaowaleta pamoja wanasiasa wote wa upinzani, umeeleza kuridhishwa na mazungumzo waliyoyafanya kati yao na mratibu wa mazungumzo ya amani, rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin William Mkapa, jijini Brussels.

Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa ambaye pia ni mratibu wa mazungumzo ya Burundi
Rais wa zamani wa Tanzania, Benjamin Mkapa ambaye pia ni mratibu wa mazungumzo ya Burundi eac.int
Matangazo ya kibiashara

Mkuu wa kitengo cha mawasiliano wa muungano huo, Jeremiah Minani, ameiambia idhaa hii kuwa, muungano wao umeridhishwa na namna mazungumzo kati yao na mratibu wa mzozo wa Burundi, rais Mkapa yalivyoenda, na kwamba kwao ni ushindi kuona muungano wao unatambuliwa baada ya kutoshirikishwa kwenye mazungumzo ya awali ya jini Arusha, Tanzania, May 21 hadi 24.

Cnared wamemueleza mratibu wa mazungumzo hayo, kutoridhishwa kwao na namna alivyoelekeza mazungumzo ya awali, na kwamba mualiko uliokuwa umetolewa ulitolewa kwa mtu mmoja mmoja, hatua ambayo iliwafanya wasusie kikao hicho kilichofanyika kwa siku nne.

Baada ya mazungumzo ya Arusha, mratibu wa mazungumzo ya amani, rais Mkapa, mara moja aliweka nia yake ya kukutana na pande ambazo hazikushiriki mazungumzo ya Arisha kwa lengo la kuwasikia na wao walikuwa na mtazamo gani kuhusu mzozo wa nchi yao kabla ya kuanza rasmi kwa usuluhishi.

Polisi wa Burundi wakipiga doria jijini Bujumbura.
Polisi wa Burundi wakipiga doria jijini Bujumbura. STRINGER / cds / AFP

Serikali ya Bujumbura, imekataa katukatu kuketi meza moja na muungano wa Cnared, ukiutuhumu muungano huo, kwa kujaribu kutatiza hali ya usalama pamoja na kuandaa mapinduzi ya kumuondoa madarakani rais Pierre Nkurunziza.

Wanadiplomasia wa Ubelgiji ambako mazungumzo haya yamefanyika, wamethibitisha kuwa rais Mkapa, alikutana na marais wa zamani wa Burundi, Sylvestre Ntibantunganya na Domitien Ndayizeye ambao wote ni wanachama wa muungano wa Cnared.

Msemaji wa muungano huo, Minani, ameongeza kuwa, wamemuomba mratibu wa mazungumzo atakapotoa mualiko mwingine, atoe mualiko kwa muungano wao wa Cnared na sio kwa mtu mmoja mmoja.

Minani amesema kuwa msimamo wao bado umeendelea kusalia kuwa ule ule, ambao wanataka ikiwa uchaguzi utafanyika kupata Serikali ya mpito, basi uchaguzi huo ufanyike bila ya uwepo wa rais Pierre Nkurunziza ambaye wanamtuhumu kwa kukiuka katiba ya nchi ya mkataba wa amani wa Arusha.

Nchi ya Burundi imejikuta ikitumbukia kwenye machafuko ya kisiasa yanayotishia kutokea kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, hali ambayo ilijitokeza baada ya rais Nkurunziza kutangaza kuwania urais kwa muhula wa tatu mfululizo, April mwaka 2015 kabla ya kuchaguliwa tena kwenye uchanguzi wa mwezi July mwaka huohuo.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.