Pata taarifa kuu
BURUNDI-UN-MACHAFUKO

Burundi: Ban Ki-moon akutana kwa mazungumzo na Pierre Nkurunziza

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon, aliwasili mjini Bujumbura, nchini Burundi Jumatatu hii alaasiri saa kumi na nusu saa za Afrika ya Kati.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura, Februari 22, 2016.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon akiwasili katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Bujumbura, Februari 22, 2016. © Griff Tapper / AFP
Matangazo ya kibiashara

Ziara hii ya siku mbili ya Ban nchini Burundi ni katika mfululizo wa jitihada za Umoja wa Mataifa wa kutafutia amani nchi ya Burundi, baada ya kukumbwa na machafuko kufuatia uamuzi wa Rais Pierre Nkurunziza wa kuwania muhula wa tatu, ambao kwa mujibu wa upinzani na mashirika ya kiraia nchini humo ni kinyume na Katiba pamoja na Mkataba wa Amani na Maridhiano wa Arusha.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa, ameletwa nchini Burundi na mambo mawili ambayo ni pamoja na kumshawishi Rais Pierre Nkurunziza kukubali bila masharti kushiriki mazungumzo na upinzani ulio uhamishoni nje ya nchi, pamoja na kuruhusu wataalam wa Umoja wa Mataifa kuendesha uchunguzi kuhusu madai ya ukiukwaji wa haki za binadamu ikiwa ni pamoja na makaburi ya halaiki ambayo yalidaiwa kugunduliwa hivi karibuni, kwa mujibu wa chanzo cha kidiplomasia cha kigeni.

Lakini ujumbe wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa unaonekana kuwa utakua na kazi kubwa nchini humoi. Nchi ya Burundi kwa sasa inakabiliwa na hali ya sintofahamu kutokana na vurugu zinazoendelea, huku serikali ya Bujumbura ikikataa mazungumzo na upinzani ulio uhamishoni nje ya nchi, pia serikali ya Bujumbura imekataa kutumwa nchini mwake kwa kikosi cha askari wa kulinda amani cha Umoja wa Afrika na maandamano yenye uchochezi wa chuki na uhasama dhidi ya Rwanda na rais wake, ambaye anatuhumiwa kulilipatishia mafunzo na kulisaidia kijeshi kundi jipya la waasi wa Burundi.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa anatarajiwa kukutana na Waziri wa Mambo ya Nje Burundi, Alain-Aimé Nyamitwe, wanasiasa, ikiwa ni pamoja na baadhi ya wanasiasa wa upinzani ambao wamebaki nchini.

Pia Ban Ki-moon atakutana Jumanne hii asubuhi na Rais Pierre Nkurunziza. Mazungumzo kati ya wawili hawa yatachukua muda wa saa moja kwa mujibu wa vyanzo vya Umoja wa Mataifa. Ban Ki-moon atajaribu kumshawishi Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza ili waeze kukubali bila masharti mazungumzo yatakayowashirikisha wadau wote.

Haki za binadamu

Wasiwasi mwingine, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa atashughulikia suala la "ukiukwaji mkubwa wa haki za binadamu nchini Burundi". "Tunaamini kwamba atafanikiwa kumshawishi rais wa Burundi kukubali uchunguzi wa kimataifa kuhusu madai hayo," alisema mwanadiplomasia mjini Bujumbura.

Leo, jamii ya kimataifa "inakaribisha ishara ndogo iliyotolewa na utawala wa Burundi kabla ya ziara hii," alisema mwanadiplomasia huyo, akimaanisha hasa kwa kufuta vibali kadhaa vya kimataifa vya kukamatwa dhidi ya wapinzani, kufungua upya vituo viwili vya redio binafsi au pia kukubaliwa kwa ujumbe wa wataalam watatu walioteuliwa na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya haki za binadamu. Kwa hiyo kila mtu ana matumaini kwamba Pierre Nkurunziza atakubali.

Hali ya taharuki katika mji wa Bujumbura

Ziara hii ya Ban Ki-moon imekuja wakati ambapo hali ya taharuki imeendelea kutanda katika mji wa Bujumbura. Mtu mmoja ameuawa na wengine zaidi ya saba walijeruhiwa katika mashambulizi mawili ya maguruneti yaliotokea Jumatatu hii asubuhi katika mji wa Bujumbura. Shambulio la kwanza limetokea mapema asubuhi katika soko la Buyenzi City Market (BCM) maarufu kwa Siyoni wilayani Ngagara. Shambulio la pili lilitokea katika soko la wilayani Kamenge, kaskazini mwa mji wa Bujumbura. Meya wa jiji la Bujumbura Freddy Mponimpa amesema kuwa "gaidi" mmoja na watu wengine wawili wanaoshukiwa kuhusiika katika mashambulizi hao wamekamatwa. "Gaidi" au "Magaidi" ni neno linalotumiwa na utawala wa Bujumbura kwa kumaanisha waasi wenye silaha.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.