Pata taarifa kuu
NIGERIA-BOKO HARAM-Usalama

Kwenye Twitter, Boko Haram yakanusha kupoiteza Baga

Jumapili jioni, mwishoni mwa juma hili lililopita kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii, Boko Haram imekanusha taarifa iliyotolewa na jeshi la Nigeria kwamba ilipoteza mji wa Baga, na kwamba ilipata hasara kubwa baada ya mji huo kuanguka mikononi mwa jeshi la serikali.

Wanajeshi wa Nigeria katika mji wa Baga. Ni vigumu kujua kwa sasa nani kati ya jeshi la Nigeria na Boko Haram anaedhibiti mji wa Baga.
Wanajeshi wa Nigeria katika mji wa Baga. Ni vigumu kujua kwa sasa nani kati ya jeshi la Nigeria na Boko Haram anaedhibiti mji wa Baga. REUTERS/Tim Cocks
Matangazo ya kibiashara

Jumamosi mwishoni mwa juma hili, jeshi la Nigeria lilitangaza kwamba liliurejesha kwenye himaya ya serikali mji wa Baga, kaskazini mashariki mwa nchi.

Mapema mwezi Januari, mji wa Baga, ulioko katika mwambao wa Ziwa Chad ulianguka mikono mwa kundi la Boko Haram, lililoendesha shambulio ambalo linaaminika kuwa ni la kwanza kuwahi kutokea kwa kipindi cha miaka sita iliyopita, ambalo lililogharimu maisha ya watu wengi.

Baada ya mapigano makali na wapiganaji wa Boko Haram, wanajeshi wa Nigeria waliurejesha mji wa Baga kwenye himaya ya serikali Jumamosi alasiri, jeshi lilitangaza kwenye akaunti yake ya Twitter.

Hasara kubwa ilitokea katika mapigano hayo, na operesheni ya kuyatafuta mabaki ya wanamgambo hao wa Boko Haram inaendelea, jeshi liliongeza.

Ndani ya kipindi cha mwezi mmoja pekee wa Januari, Boko Haram iliyateka baadhi ya maeneo ya Nigeria, hususan, kambi ya kikosi cha wanajeshi wa kimataifa katika mji wa Baga, kilomita chache kutoka Ziwa Chad, pamoja na mji wa Monguno.

Mji wa Monguno, kusini mashariki mwa Nigeria, ulianguka mikononi mwa kundi la Boko Haram Jumapili Januari 25 mwaka 2015 asubuhi, baada ya mapigano makali kati ya jeshi na wapiganaji wa kundi hilo la Boko Haram.

" Mji wa Baga uko mikono mwa Mujahideen, wanajeshi wa Mwenyezi Mungu. Madai yoyote yanayotolewa na maadui kwamba mji wa Baga umedhibitiwa na jeshi ni uzushi mtupu", kundi la Boko Haram limesema kwenye mtandao wa Twitter.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.