Pata taarifa kuu
DRC-BENI-ADF-Usalama

Watu 37 wauawa Beni, ADF-Nalu yanyooshewa kidole

Usiku wa Jumamosi Desemba 6 kuamkia Jumapili Desemba 7, watu wenye mapanga wanaoshukiwa kuwa waasi wa ADF-Nalu, kwa mujibu wa viongozi tawala , walishambulia vijiji 3 wilayani Beni mashariki mwa jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kuwaua watu 37 na kumjeruhi mtu mmoja.

Raia wa mji wa Beni wameanza kuukimbia mji huo kufuatia shambulio la waasi wa Uganda wa ADF-Naluusiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili Desemba 7 mwaka 2014, shambulio ambalo limegharimu maisha ya watu zaidi ya 37.
Raia wa mji wa Beni wameanza kuukimbia mji huo kufuatia shambulio la waasi wa Uganda wa ADF-Naluusiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili Desemba 7 mwaka 2014, shambulio ambalo limegharimu maisha ya watu zaidi ya 37. AFP/Alain Wandimoyi
Matangazo ya kibiashara

Kwa mujibu wa vyanzo vya RFI watu 37 waliuawa katika mashambulizi hayo, ambayo yanadaiwa kutekelezwa na waasi wa Uganda wa ADF-Nalu wanaoendesha harakati zao Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Mashirika ya kiraia mkoani Kivu Kaskazini yamesema kusononeshwa na mauaji hayo, ambayo yametimiza idadi ya watu 250 kuuawa wilayani Beni kwa kipindi cha miezi miwili. Watu zaidi ya 20,000 wameyahama makazi yao.

Mashirika ya kiraia yametolea wito vikosi vya usalama vya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na tume ya Umoja wa Mataifa nchini Congo Monusco kushirikiana kwa pamoja ili kukomesha mauaji na vitisho ambavyo vinaendelea kushuhudiwa katika eneo hilo. Wito huo umekaribishwa na tume ya Umoja wa Mataifa Monusco kupitia msemaji wake Charles Bambara, hata kama operesheni hiyo bado haijaanza.

Hayo yanajiri wakati ambapo serikali mpya ya "mshikamano wa kitaifa" imeundwa tangu Jumapili Desemba 7. Timu hii imekua inatarajiwa kwa zaidi ya mwaka mmoja. Watu watatu wameteuliwa kushikilia nyadhifa za manaibu Mawaziri wakuu katika serikali hiyo ikiwa ni pamoja na Evariste Boshab, katibu mkuu wa chama cha PPRD, ambaye atahusika na mambo ya ndani. Thomas Luaka, katibu mkuu wa chama cha MLC, atahusika na masuala ya uchukuzi na mawasiliano (PTT). Willy Makiashi, kutoka chama PALU, atahusika na masuala ya ajira. Serikali hiyo mpya inakabiliwa na changamoto zinazolikabili taifa la Congo wakati huu, kama vile ukosefu wa usalama katika mikoa ya mashariki.

Alexis Thambwe Mwamba, ameteuliwa kuwa Waziri wa sheria. Mwaka 2008 alikua Waziri wa mambo ya nje.
Alexis Thambwe Mwamba, ameteuliwa kuwa Waziri wa sheria. Mwaka 2008 alikua Waziri wa mambo ya nje. AFP PHOTO BERTRAND GUAY

Wakati huohuo mvutano unaendelea kujitokeza kuhusu kugombea kwa rais Joseph Kabila Kabange katika uchaguzi wa urais utakaofanyika mwaka 2016. Kulingana na Katiba ya Congo , Kabila hapaswi kugombea baada ya kutimiza idadi ya mihula miwili. Lakini mijadala imekua ikifanyika ili kufanya marekebisho ya Katiba yanakayompa nafasi rais Kabila aweze kugombea kwa muhula watatu.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.