Pata taarifa kuu
BURUNDI-UPINZANI-CENI-UTAWALA-SIASA-USALAMA

Burundi : kasoro zaanza kujitokeza kwenye zoezi la uandikishaji

Mvutano kuhusu zoezi la kuandika wapiga kura nchini Burundi umeanza kuibuka kati ya vyama vya upinzani na tume huru ya uchaguzi kufuatia kasoro ambazo zimeanza kujitokeza katika zoezi hilo.

Raia mjini Bujumbura hawajitokezi kwa wingi katika zoezi la kujiorodhesha kwenye daftari la wapiga kura.
Raia mjini Bujumbura hawajitokezi kwa wingi katika zoezi la kujiorodhesha kwenye daftari la wapiga kura. Esdras Ndikumana / AFP
Matangazo ya kibiashara

Mvutano huo umesababishwa na kugunduliwa kwa vyeti bandia vya uraia katika baadhi ya vituo vya uandikishaji mjini Bujumbura. Baadhi ya vyeti hivyo vilikua havina muhuri, huku katika maeneo mengine ya nchi kukionekana vijana wakihamasisha raia kutoshiriki zoezi hilo.

Aliyekuwa makamu wa rais, Frédérick Bamvuginyumvira, ambaye ni naibu kiongozi wa chama cha upinzani cha Sahwanya-Frodebu amesema kasoro hizo ambazo zimeanza kujitokeza katika zoezi la uandikishaji ni ishara ya wizi wa kura ambao umepangwa kufanyika katika uchaguzi wa hapo mwakani, huku akiinyooshea kidole tume huru ya uchaguzi kwamba huenda inahusika katika mpango huo.

Bamvuginyumvira ameiomba tume huru ya uchaguzi kuanzisha mazungumzo na vyama vyote vya siasa ili kujadili hali hiyo na kuitafutia ufumbuzi haraka iwezekanavyo.

Kwa upande wake tume huru ya uchaguzi kupitia msemaji wake, Prosper Ntahogwamiye amebaini kwamba kasoro zinazojitokeza katika zoezi hilo zitapatiwa ufumbuzi haraka iwezekanavyo. Ameomba vyama vya upinzani kuwa na imani na tume huru ya uchaguzi.

Raia katika maeneo mbalimbali nchini Burundi wakisema kutiwa wasiwasi na uchaguzi wa mwaka 2015.
Raia katika maeneo mbalimbali nchini Burundi wakisema kutiwa wasiwasi na uchaguzi wa mwaka 2015. Sébastien Németh/RFI

Hayo yanajiri wakati ambapo idadi ya watu wanaojiorodhesha  kwa siku ni ndogo ikilinganishwa na zoezi la uandikishaji la mwaka 2009 kabla ya uchaguzi wa mwaka 2010. Zoezi hili ambalo limeanza Jumatatu Novemba 24 litadumu majuma mawili.

Pacifique Nininahazwe, kiongozi wa muungano wa mashirika ya kiraia Focode.
Pacifique Nininahazwe, kiongozi wa muungano wa mashirika ya kiraia Focode. AFP PHOTO/ROBERTO SCHMIDT

Wakati hayo yakijiri, muungano wa mashirika ya kiraia Focode, umeelezea wasiwasi wake kufuatia vitisho vya kuuawa anavyofanyiwa kiongozi wa muungano huo, Pacifique Nininahazwe. Katibu mkuu wa Focode, Janvier Bizimana, amesema kuna watu ambao wamekua wakijielekeza nyumbani kwa Pacifique Ninahazwe na kuanza kufanyia vitisho familia yake. Janvier Bizimana ameiomba serikali kuzingatia usalama wa Pacifique Ninahazwe.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.