Pata taarifa kuu
SUDAN-SUDAN KUSINI-ABYEI

Kura ya maoni yaingia siku ya pili katika jimbo la Abyei, huku rais Bashir akiahidi suluhu

Rais wa Sudan Omar al Bashir ameahidi kupata suluhu ya mgogoro wa eneo la Abyei huku wenyeji wa jimbo hilo kwa siku ya pili wakipiga kura ya maoni kuamua mustakabali wa jimbo hilo.

Matangazo ya kibiashara

Kabila la Dinka Ngok ndilo linaloshiriki katika zoezi hilo ambalo linataka eneo hilo kuwa Sudan Kusini lakini kabila la Misseriya likitaka jimbo hilo kusalia nchini Sudan.

Ripoti kutoka Abyei zinasema kuwa matokeo ya kura hiyo ya maoni yanatarajiwa kufahamika tarehe 31 mwezi huu wa Oktoba kwa mujibu wa Kamati andalizi inayosimamia kura hiyo.

Msemaji wa Kamati hiyo Luka Biong,  amesema kuwa kwa siku ya pili leo zoezi hilo linakwenda kama lilivyopangwa na watu wa Kabila la Ngok Dinka wapatao 100,000 wamerudi nyumbani kushiriki katika kura hiyo.

Mmiliki hasa wa eneo la Abyei linasalia tata baada ya kukosa ufumbuzi kutokana na makubaliano ya amani ya 2005 yaliyoweka mikakati ya Sudan na Sudan Kusini Kusini kujitenga.

Makubaliano hayo ya amani yaliyofikiwa jijini Nairobi nchini Kenya yaliweka wazi kuwa wakaazi wa Abyei walistahili kupiga kura siku moja raia wa Sudan Kusini mwaka 2011 kutaka kujitenga kwao lakini hilo halikufanyika.

Hata hivyo, kura hii ya maoni ya Abyei haitambuliwi na Umoja wa Afrika, Sudan na Sudan Kusini kwa sababu hakuna makubaliano yoyote yaliyofikiwa kufanyika kwa kura hiyo ya maoni kwa watu wa Abyei kuamua wanataka kuwa raia wa nchi gani.

Wiki iliyopita, rais wa Sudan Omar Al Bashir alizuru Sudan Kusini kuzungumzia hatima ya Abyei na mwenyeji wake rais Salva Kiir bila mafanikio baada ya viongozi hao wawili kushindwa kuafikiana tarehe ya kufanyika kwa kura hiyo.

Umoja wa Afrika mwaka uliopita ulipendekeza kuwa kura hiyo ya maoni ifanyike mwisho wa mwezi huu lakini Juba na Khartoum zimeshindwa kuafikiana ikiwa watu wa kabila la Miseriya wanastahili kushiriki katika zoezo hilo au la.

Serikali ya Sudan inashikilia msimamo kuwa ni sharti jamii ya watu wa Miseriya wanaohamahama waruhusiwe kushiriki katika kura hiyo ya maoni, suala ambalo serikali ya Sudan Kusini inapinga na kusema ni watu wa Kabila la Dinka Ngok ndio wanaotashili kuamua mustakabali wao.

Wakati hayo yakijiri, Umoja wa Afrika unasema kuwa umesikitishwa na hatua ya serikali ya Sudan kuwazuia wajumbe wake kuzuru Abyei mwishoni mwa juma lililopita kwa madai kuwa iliyokuwa ni kwa sababu za kiusalama.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.