Pata taarifa kuu
SUDAN

Rais Bashir asema maandamano ya mwezi uliopita yalilenga kuipindua serikali

Rais wa Sudan Omar al Bashir amesema kuwa maandamano yaliyofanyika nchini humo mwezi uliopita yalikuwa ni mojawapo ya mkakati wa kumwondoa madarakani.

Matangazo ya kibiashara

Akilihutubia taifa kupitia Radio ya Taifa, rais Bashir ameongeza kuwa baada ya serikali yake kutangaza hatua ya kuondoa ruzuku ya mafuta kwa ajili ya kuimarisha uchumi wa taifa hilo, wapinzani waliokuwa na lengo la kuingusha serikali yake waliwatuma wezi na makundi ya watu ambao amewataja maadui wa Sudan kufikia lengo hilo.

Rais huyo ambaye pia aliingia uongozini kupitia mapinduzi ya kijeshi mwaka 1989 amesema kuwa Sudan inalindwa na Mungu na hakuna anayeweza kumpindua na kumwondoa madarakani.

Kiongozi huyo wa Khartoum inasema kuwa upinzani pia ulitumia mamluki kutoka nje kudhoofisha usalama nchini humo madai ambayo viongozi wa maandamano hayo wamekanusha na kusema wananchi wa sudan ndio waliojitokeza baada ya kubaini kuwa serikali ilikuwa imewabebesha mzigo.

Mwezi uliopita, Serikali ya Khartoum iliondoa ruzuku ya mafuta na kusababisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kupanda kwa asilimia 60 na kusababisha maandamano makubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa dhidi ya uongozi wa Bashir.

Uchumi wa Sudan umekuwa ukiyumba tangu mwaka 2011 baada ya kujitenga kwa Sudan Kusini kutokana na taifa hilo jipya kusalia na visima vingi vya mafuta na hivyo Sudan kukosa sehemu ya kuchuma riziki kama ilivyokuwa awali.

Serikali ya Sudan inasema kuwa idadi ya watu waliopoteza maisha yao katika maandamano hayo ni kati ya 60 na 70 idadi ambayo inakanushwa na mashirika ya Kimataifa ya kutetea haki za binadamu ambayo inasema zaidi ya watu 200 waliuawa na mamia kujeruhiwa.

 

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.