Pata taarifa kuu
UFARANSA-UGAIDI

Ufaransa: Rais Macron alaani tukio la utekaji Trebes, watu 3 wauawa

Watu watatu wamepoteza maisha na wengine kadhaa wamejeruhiwa nchini Ufaransa katika tukio la utekaji lililofanywa na mtu mmoja aliyekuwa na silaha kwenye duka moja la jumla kwenye mji wa Trebes kusini mwa Ufaransa ambapo aliwashikilia mateka watu kadhaa na kuthibitisha kuwa mfuasi wa kundi la Islamic State.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron. REUTERS/Francois Lenoir
Matangazo ya kibiashara

Vyombo vya usalama vimemuua mtekaji ambaye anaaminika kuwa na asili ya Morocco na alikuwa kwenye orodha ya watu waliokuwa wakifuatiliwa kwa kuwa washirika wa kundi la Islamic State.

Kabla ya kuwateka watu kwenye duka la jumla mtuhumiwa huyo alitekeleza mashambulizi matatu tofauti kwenye mji wa Carcassonne na jirani na kitongoji cha Trebes.

Mtu huyo kwa mara ya kwanza aliiba gari kwa nguvu kwenye mji wa Carcassonne na kumuua mmoja wa abiria na kumjeruhi dereva kabla ya kumpiga risasi polisi ambaye alikuwa akifanya mazoezi na wenzake.

Baada ya hapo aliendesha gari hadi kwenye duka la jumla la Super U kwenye mji wa Trebes na kujificha kwa zaidi ya saa tatu akiwa na mateka wake, akiua watu wawili.

Polisi wakiwa wamezuia njia ya kuingia Trebes wakati wa zoezi la kujaribu kuwaokoa mateka kwenye duka la jumla. 23 Machi 2018
Polisi wakiwa wamezuia njia ya kuingia Trebes wakati wa zoezi la kujaribu kuwaokoa mateka kwenye duka la jumla. 23 Machi 2018 ERIC CABANIS / AFP

Mtu aliyemuona mtuhumiwa huyo kwa mara ya kwanza amedai alikuwa amejihami kwa visu, bunduki na mabomu na alikuwa akitamka maneno Allahu Akbar kabla ya kungia ndani ya duka hilo.

“Mtu huyo alianza kupiga kelele na kuanza kufyatua risasi kadhaa,” mteja mmoja wa duka hilo alikiambia kituo cha FranceInfo.

“Niliona mlango uliowazi na ulikuwa ni wa jokofu na nikawaambia watu wote tuingie humo,” alisema shuhuda huyo.

Baada ya kuwaachia mateka mtuhimiwa alisalia peke yake na polisi mmoja, sambamba na aisa mwingine ambaye alipigwa risasi wakati kikosi maalumu cha kupambana na ugaidi kilipovamia ndani ya jengo.

Mauaji haya yamekuja wakati huu nchi ya Ufaransa ikiwa kwenye hali ya tahadhari baada ya matukio mengine ya kigaidi tangu mwaka 2015.

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron ametoa pole kwa familia zilizopoteza wapendwa wao pamoja na wale waliojeruhiwa ambapo amesema anarejea jijini Paris kutokea Brussels alikokuwa akihudhuria mkutano wa wakuu wa nchi za umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Gerard Collomb alitembelea eneo la tukio na kuthibitisha kuuawa kwa mshambuliaji pamoja na kujeruhiwa kwa polisi kadhaa ambao walibadilishana na mateka.

Tayari waendesha mashtaka wa masuala ya ugaidi wa Paris wameanza uchunguzi kuhusiana na tukio hili ambalo wamesema wanalichukulia kama tukio la kigaidi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.