Pata taarifa kuu
UTURUKI-UHOLANZI

Erdogan: Ilichofanya nchi ya Uholanzi kitawagharimu

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdogan, Jumapili ameionya nchi ya Uholanzi akisema nchi hiyo itajutia uamuzi iliyoufanya wa kuwazuia mawaziri wake, kufanya mikutano ya kuwashawishi raia wa Uturuki wanaoishi ughaibuni kupiga kura ya ndio wakati wa kura ya maoni kuhusu marekebisho ya katiba.

Rais wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan, akizungumza jijini Instanbul. Machi 11, 2017.
Rais wa Uturuki, Racep Tayyip Erdogan, akizungumza jijini Instanbul. Machi 11, 2017. ©Kayhan Ozer/Presidential Palace/Handout via REUTERS
Matangazo ya kibiashara

Matamshi ya Erdogan yamekuja wakati nchi ya Uturuki ikiendelea kuvutana vikali na nchi washirika za Ulaya, hali inayotishia uwezekano wa nchi hiyo kukubaliwa kuwa mwanachama wa umoja wa Ulaya.

Rais Erdogan amerejelea matamshi yake tata aliyoyatoa mwishoni mwa juma, akiituhumu Uholanzi ambayo ilitawaliwa na watawala wa Kinazi wa Ujerumani wakati wa vita ya pili ya dunia, kuwa inafanya mambo kama mbaguzi kutokana na kile ilichowafanyia mawaziri wake.

Wachambuzi wa mambo wanatabiri kuwa kura ya safari hii itakuwa ngumu kwa kambi zote ifikapo April 16 mwaka huu kuhusu marekebisho ya katiba, huku mawaziri wake wakiendelea kufanya mikutano zaidi kwenye miji mikubwa ya nchi za umoja wa Ulaya.

Hii imekuja baada ya waziri wa familia wa Uturuki, Fatma Betul Sayan Kaya, kuzuiliwa kuhutubia moja ya mikutano aliyokuwa amepanga kwenye mji wa Rotterdam, ambapo alisindikizwa na polisi hadi kwenye mpaka wa nchi hiyo na Ujerumani.

Hivyohivyo mwishoni mwa juma, Serikali ya The Hague ilimkatalia waziri wa mambo ya kigeni wa Uturuki, Mevlut Cavusoglu kufanya moja ya mikutano kama hiyo.

Rais Erdogan amenukuliwa na vyombo vya habari akisema "Uholanzi!! ikiwa unajitoa muhanga kuharibu uhusiano wa wadachi na waturuki kwaajili ya uchaguzi tu, suala hili litawagharimu," alisema Erdogan aliyekuwa anaonekana kuwa na hasira wakati akizungumza mjini Instanbul, akizungumzia uchaguzi wa Machi 15 nchini Uholanzi.

"Watajifunza nini maana ya diplomasia," akiongeza kuwa "kilichotokea kamwe hakiwezi kuachwa bila kujibiwa".

Erdogan amekariri tuhuma zake kwa kilichotokea siku ya Jumamosi nchini Uholanzi, akisema tabia iliyoonesha ni ya Kinazi na Kibaguzi.

Akizungumza kwenye mji wa Metz nchini Ufaransa, ambako mkutano wao uliruhusiwa kuendelea, waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Cavusoglu, ameitaja nchi ya Uholanzi kama nchi ya Kibaguzi.

Katika hatua nyingine, waziri mkuu wa Denmark Lars Lokke, ametoa wito kwa mwenzake wa Uturuki, Binali Yilirim, kuahirisha kwa muda mpango wake wa kufanya mkutano wa hadhara na wananchi wa Uturuki wanaoishi nchini humo, akisema kufanya mkutano huo wakati huu sio muafaka.

Waziri mkuu Lokke amesema mkutano huo hauwezi kufanyika huku Uturuki ikitoa matamshi ya uchochezi dhidi ya Uholanzi.

Kusambaza :
Ukurasa haipatikani

Maudhui unayojaribu kuyatafuta hayapatikani kwa sasa au yamekwishaondolewa.