Ufaransa: Waandamanaji elfu moja wamekamatwa, ghasia zaidi zikiripotiwa
Nairobi – Matukio ya ghasia na uporaji yameshuhudiwa kwa usiku wa nne wa maandamano nchini Ufaransa wakati huu maofisa wa polisi wakithibitisha kukamatwa kwa watu elfu moja wanaoandamana kufuatia kifo cha kijana aliyeuawa na afisa wa usalama katika kituo cha trafiki.
Imechapishwa: Imehaririwa:
Kwa mujibu wa serikali, ghasia hizo "zimepungua" ikilinganishwa na usiku uliopita, lakini wizara ya mambo ya ndani bado iliripoti kukamatwa kwa watu 994 kote nchini kwa usiku mmoja, na majeruhi 79, polisi na askari wakiwa miongoni mwao.
Maandamano nchini humo yaliaanza siku ya Jumanne, baada ya kuchochewa na kifo cha Nahel mwenye umri wa miaka 17 ambaye alipigwa risasi na afisa wa polisi.
Mamlaka nchini humo katika taarifa yake imeeleza kuwa licha ya kuripotiwa kwa majeruhi katika maandamano hayo, magari 1,350 na majengo 234 yamechomwa moto.
Makabiliano yameripotiwa licha ya Ufaransa kuwatuma maafisa 45,000, hii ikiwa ni idadi kubwa zaidi kutumwa kuwakabili waandamanaji.
Waandamanaji wameripotiwa kupora mali katika miji ya Marseille, Lyon na Grenoble ambapo pia ghasia zaidi zimeripotiwa.
Timu ya taifa ya soka ya Ufaransa nayo pia imetoa wito kwa kusitishwa kwa vurugu zinazoendelea kushuhudiwa.