Macron aendelea kupata pongezi mbalimbali kutoka kwa viongozi duniani
Viongozi mbalimbali duniani, wamempongeza rais Macron kwa ushindi alioupata. Miongoni mwa pongezi hizo zimetoka barani Ulaya kutoka kwa rais wa Tume ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen na rais wa Baraza hilo Charles Michel ambao wamesma wana uhakika wa ushirikiano wa Ufaransa miaka metano ijayo.
Imechapishwa:
Kansela wa Ujerumanu Olaf Scholz naye amesema kwa ushindi wa Macron, wapiga kura nchini Ufaransa wametuma ujumbe, kuwa wanaiamini Umoja wa Ulaya.
Rais wa Marekani Joe Biden naye amemwambia Macron kuwa, anatumai kuendeleza ushirikiano kati ya mataifa hayo mawili, ujumbe kama huo pia ukitoka kwa Xi Jinping wa China.
Salamu za pongezi pia zimetoka kwa rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky ambaye amesema ana imani kuwa wataendeleza ushirikiano ili kupata ushindi.
Naye rais wa Urusi Vladimir Putin kupitia ukurasa wake wa Telegram, amempongeza Macron na kumtakia afya njema.
Viongozi wa mataifa ya Afrika, wakiongozwa na rais wa Senegal ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika Macky Sall , Paul Kagame wa Rwanda, Samia Suluhu Hassan wa Tanzania, Waziri Mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed ni miongoni mwa viongozi waliompongeza Macron kwa ushindi aliopata.